Balozi wa Utalii Bi Isabela ahimiza kuboreshwa miundombinu ya Barabara Hifadhi ya Ruaha
21 March 2022, 6:57 am
Balozi wa Utalii Nchini Tanzania Isabela Mwampamba ameishauri serikali kutengeneza miundombinu ya barabara ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kutoka iringa Mjini.
Balozi Isabela ameyasema hayo mara baada ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwenye ziara ya wanawake kutoka taasisi mbalimbali za mikoa ya nyada za juu kusini na kuongeza kuwa endapo miundombinu itarekebishwa itasaidia kuongeza watalii.
Balozi Isabela amesema kuwa ana wajibu wa kuhamasisha wadau wengine hasa wanawake kuwa na mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii.
Naye Amina Rashid Afisa uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha amekiri kuwepo na changamoto ya miundombinu ya barabara ambapo tayari serikali imeanza mchakato wa kutatua changamoto hiyo.
Kwa upande wao Tully Kulanga afisa utalii kutoka Ofisi ya Utalii Kanda ya nyanda za juu kusini na Hoza Mbura kutoka Bodi ya Utalii Kanda ya Iringa wamesema kuwa ziara ya kutembelea hifadhi itakuwa kichocheo cha kukuza utalii wa ndani.
Akijibia kuhusu changamoto ya Miundombinu ya barabara ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amesema kuwa serikali inatambua changamoto hiyo na itatenga fedha katika kipindi cha bajeti kwa ajili ya kutengeneza barabara kwa kushirikiana na Benki ya dunia na wadau wengine.
Ziara ya wanawake kutoka Taasisi za Nyanda za Juu Kusini ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imeandaliwa na Wizara ya Utalii kupitia Bodi ya Utalii kanda ya Iringa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Milaya ya Iringa na Balozi wa Utalii nchini Tanzania Isabela Mwampamba