DC Kheri aagiza ukarabati wa soko kuu Iringa
21 March 2024, 9:48 am
Siku chache baada ya soko kuu la Iringa kuruhusiwa kufanya biashara mpaka saa nne usiku, Mkuu wa Wilaya ya Iringa ameagiza utekelezaji wa kukarabati miundombinu ya soko hilo.
Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa wilaya ya Iringa Kheri James ameilekeza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuanza haraka utekelezaji wa mpango wa ukarabati wa soko kuu ili kuwezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika sehemu salama.
Mh. Kheri James ametoa maelekezo hayo mapema leo, baada ya kutembelea soko kuu kwa lengo la kukagua hali ya miundombinu, huduma na kuzungumza na wafanyabiashara katika soko hilo.
Katika ziara hiyo wafanyabiashara wa soko kuu wamemueleza Mheshimiwa Mkuu wa wilaya changamoto mbalimbali zinazo kabili soko hilo, changamoto kubwa ikiwa ni kuvuja kwa paa hali inayopelekea uharibufu wa mali na bidhaa katika soko hilo.
Kheri ameeleza kuwa ni jukumu la Halmashauri kupanga na kusimamia ustawi wa biashara katika mji ikiwa ni pamoja na kutekeleza kwa wakati mipango inayo chochea ukuaji wa biashara na ustawi wa wafanyabiashara wenyewe.
Mkuu wa wilaya anatarajia kuendelea na ziara ya kutembelea, kukagua na kufatilia hali ya miundombinu, huduma katika maeneo yote yanayo hudumia wananchi wilayani Iringa.