Nuru FM
Nuru FM
13 April 2026, 09:27

Viongozi wa Serikali za Vijiji wametakiwa kuwashirikisha wananchi wao kujadili kuhusu umuhimu wa Mango wa chakula shuleni.
Na Hafidh Ally
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh. Kheri James, amewaagiza Viongozi wa Serikali za vijiji kuweka agenda ya kusimamia mpango wa utoaji wa chakula shuleni katika mikutano yao ili kukabiliana na changamoto ya udumavu na utapiamlo kwa watoto.
Mh. Kheri ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Shule ya Sekondari ya Irole iliyopo Wilaya ya Kilolo, iliyolenga kutembelea na kukagua maendeleo ya miradi ya elimu na kuongeza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa vijiji, walimu na wazazi una nafasi kubwa ya kuchochea mafanikio ya programu ya utoaji wa chakula shuleni.
Mh. Kheri amesema kuwa endapo watoto watapata fursa ya kupata chakula shuleni itasaidia kuboresha ufaulu wa wanafunzi, kupunguza utoro na kuongeza ari ya kujifunza.
“Mtoto anayepata lishe bora huwa na uwezo mkubwa wa kuelewa na kufanya vizuri katika masomo yake ndiyo maana tunasisitiza uwepo wa matunda katika chakula cha wanafunzi,” Alisema Kheri
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Bi. Siwema Juma, amesema kuwa halmashauri hiyo itaendelea kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora ili kuongeza uelewa wao darasani na kuboresha matokeo ya kitaaluma.
Awali Diwani Kata ya Irole Eriki Kikoti amesema kuwa atahakikisha anawahamasisha wenyeviti wa Vijiji katika Kata yake wanatekelea agizo la Mh Mkuu wa Mkoa kutoa elimu ya umuhimu wa Mzazi kuchangia Chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameishukuru serikali kwa juhudi za kuimarisha mazingira ya kujifunzia pamoja na huduma za chakula shuleni, wakisema hatua hizo zinawasaidia kujifunza kwa ufanisi zaidi.