Nuru FM

Wanafunzi Iringa wapewa Unga wa lishe

5 February 2026, 10:20 am

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta akikabidhi Unga wa Lishe. Picha na Hafidh Ally

Mpango wa lishe shuleni kupitia mkataba wa lishe ulioasisiwa mwaka 2022, unawataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye virutubisho vya kutosha.

Na Hafidh Ally

Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupitia mapato yake ya ndani imefanikiwa kugawa jumla ya Kilo  900 ya unga lishe kwa shule tano ili kukabiliana na changamoto ya udumavu kwa watoto.

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa chakula hicho kwa shule hizo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amesema amefurahishwa na mpango wa Manispaa ya Iringa kuanza kwa vitendo utekelezaji wa afua za lishe.

Sauti ya Sitta

“Lengo la Mhe. Rais ni kuwa na taifa la watu wenye afya bora. Ndiyo maana mikataba hii imesainiwa na utekelezaji unaendelea kwa kushirikiana na halmashauri. Huu unga wa lishe tuliogawa leo ni sehemu ya kuhakikisha kila mtoto, bila kujali mchango wa mzazi, anapata uji wenye virutubisho muhimu, ikiwemo Vitamin A kwa ajili ya uoni na afya ya macho,” alisema Mhe. Sitta.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Bi. Zaina Mlawa, alisema manispaa imetenga fedha kutoka posho za vikao na mapato ya ndani ili kuunga mkono juhudi za serikali na wazazi katika kuboresha lishe shuleni.

Sauti ya Mlawa

Naye Afisa Lishe wa Manispaa, Bi. Anzaeli Msigwa, alieleza kuwa unga huo una faida nyingi ikiwemo kuongeza hamu ya kula, kuimarisha kinga ya mwili, na kuimarisha uoni kutokana na wingi wa Vitamin A.

Sauti ya Anzael

Hivi sasa asilimia 70 ya wanafunzi wa Manispaa ya Iringa wanapata chakula shuleni.