Barabara ya Mafinga- Mtwango yatengenezwa
22 April 2024, 10:39 am
Kukarabatiwa kwa Barabara ya Mafinga- Mtwango ambayo imekuwa ikitumiwa na wakazi wa eneo hilo katika shughuli za kiuchumi imekuwa mkombozi.
Na Tumain Msowoya
Serikali imenza kutengeneza Eneo la Barabara ya Mafinga – Mtwango lililokuwa na utelezi hadi kusababisha magari kukwama yakiwamo ya wagonjwa.
Hayo yamezungumzwa na Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihenzile wakati akiwaeleza wakazi wa Mufindi kupitia kundi la WhatsAPP la Mufindi Kwetu, kuwa tayari wamefanyia kazi kero hiyo kwa kuanza kujaza vifusi na kuanza kupitika kwa urahisi.
Kihenzile amesema Mafinga – Mtwango ni moja ya barabara muhimu kwa uchumi wa Wilaya ya Mufindi kutokana na kusafirisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara ikiwamo chai na mazao ya misitu.
Awali, baadhi ya wananchi walirekodi video iliyokuwa inaonyesha gari la wagonjwa likivutwa bila mafanikio eneo la Mtwango, Kata ya Sawala, Wilayani Mufindi.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Yudas Msangi amesema Mafinga – Mtwango ni barabara iliyopo kwenye mpango wa kuwekwa lami mwaka huu.
Amesema kwa siku zaidi ya maroli 30 yamekuwa yakipita barabara hiyo kuelekea Kiwanda cha Mgololo na viwanda vingine.