Madereva Iringa washangaa kivuko kuondolewa
7 March 2024, 4:40 pm
Kuondolewa kwa kivuko Cha katika stendi ya zamani Iringa kumetajwa kuwa sababu ya ongezeko la foleni na magari yao kuharibika.
Na Godfrey Mengele
Madereva wanaotumia kituo cha stendi kuu ya zamani, kwa sasa ikifahamika kama stendi ya daladala wameshangazwa na kitendo cha halmashauri ya manispaa ya iringa kuondoa kivuko kilichokuwa kinatumika kwa usafiri huo kwa kigezo cha kukifanyia marekebisho lakini mpaka sasa yapata mwezi wa 3 hakijarudishwa na kusababisha adha kubwa kutumika njia isiyotakiwa.
Wakizungumza na Nuru Fm kupitia kipindi cha Nyambizi madereva hao wamesema kutokana na kivuko hicho kuondolewa hivi sasa wanatumia njia ambayo wakati mwingine inasababisha foleni na hata kupigwa faini na Jeshi la polisi kwa kupaki muda mrefu ili kupisha usafiri mwingine upite unaopaswa kutumia njia hiyo.
Madereva hao wameenda mbali na kuhoji kulikuwa na ulazima gani kukiondoa kivuko hicho wakati halmashauri haikujipanga kukirejesha mapema kwani wakati kinatumika hakijawahi kuleta madhara yoyote ambayo kwa sasa kutumia njia isiyotakiwa ambayo inatumika kwa ajili ya maegesho ya usafiri mwingine na kuwepo kwa kona kali kunasababisha baadhi ya vifaa kwenye magari yao kuharibika.
Akitolea ufafanuzi juu ya kadhia hiyo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada amesema uwepo wa changamoto hiyo umesababishwa na uzembe wa baadhi ya wahusika ambao (hakuwataja wahusika hao) hivyo ametaka madereva hao kuwa na subira jambo hilo linafanyiwa kazi ndani ya muda mfupi kivuko hicho kitaweka ili kiendelea na matumizi kama ilivyo kuwa awali.