Shule ya msingi Njiapanda yanufaika na mradi wa ‘kizazi hodari’
20 November 2023, 9:46 am
Na Godfrey Mengele
Shule ya msingi njiapanda iliyopo kata ya Mwangata Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mkoani Iringa imenufaika na mradi wa kizazi Hodari unaotekelezwa na USAID kanda ya kusini wenye lengo la kuwasaidia Watoto yatima wanaoishi na maambukizi ya virusi ukimwi, Pamoja na elimu ya utambuzi kwa Watoto wa kike na kiume.
Hayo yamezungumzwa na Mwl Mkuu wa Shule ya Msingi Njiapanda Tatu Kisai katika kusherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa ufadhili wa dawa za ARVs kutoka Marekani mbele ya Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Craig Hart ambapo Mkuu huyo wa shule ya msingi Njiapanda amebainisha kuwa waliupokea vizuri mradi huo wa kizazi Hodari kwa ajili ya utekelezaji ambapo wanafunzi wa kike na kiume Pamoja na walimu walipokea mafunzo mbali.
“..Tuliupokea vizuri Mradi huu wa Kizazi Hodari Kanda ya Kusini kwa uaminifu, mpaka sasa unatekelezwa kwa afua mbili muhimu ambapo kwa watoto wa kike [Dreams] na watoto wa kiume [Coaching Boys Into Men CBIM ] na walimu wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike wanaowasimamia wanafunzi hao walipewa mafunzo kutoka Shirika la Afya la Women group kwa ufadhili wa USAID..”
Katika hatua nyingine Mwl Mkuu Tatu Kisari amebainisha kuwa katika utekelezaji wa mradi huo wamepata mafanikio makubwa kwa mwaka 2022-2023 kwa kushirikiana na Shirika la afya women group kupitia usimamizi wa Shirika la DELOITTE kwa ufadhili wa USAID waliendesha mafunzo kwa wanafunzi wa kike [Dreams] 235 na wanafunzi wa kiume CBIM 205 ambapo kupitia mafunzo hayo yamewaongezea uwezo wanafunzi hao wa kijitambua, kujieleza na kuongeza uwezo wa ufaulu kwa watoto wa kike ambao walikuwa wanakoa masomo hasa kipindi cha hedhi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Craig Hart ameipongeza shule hiyo Pamoja na wasimamizi wa mradi huo kuusimamia vizuri ili kufikia malengo yanayotarajiwa.
“…Ni fedha nyingi zilzowekezwa nchini Tanzania ambapo jumla ya sh bilioni 6 zimewekezwa kupitia miradi mbalimbali hivyo kwa kusheherekea miaka 20 ya PEPFAR Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan usimamizi wa miradi mikubwa unaonekana vilevile tutaendelea kushirikiana kufadhili kupitia miradi mingine ili kupata jamii jamii yenye ustawi mzuri…”