Waziri Mkuu Majaliwa Achangia Milion Tano Kwa Walemavu Wa Lulanzi Wilayani Kilolo
6 May 2022, 5:29 am
Waziri Mkuu wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa amechangia shilingi Milioni Tano kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili walemavu watatu wa familia Moja katika kijiji cha Lulanzi kilichopo Kata ya Nyalumbu Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa.
Akizungumza wakati wa harambee ya kuwachangia walemavu hao iliyoasisiwa na Balozi wa Utalii Tanzania Bi Isabela Mwampamba iliyofanyika katika Ofisi za kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Mbunge wa jimbo la Kilolo Mh. Justine Nyamoga amesema kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki kutoa fedha hizo baada ya kupewa taarifa za uhitaji wa walemavu hao.
Harambee hiyo imechagizwa na Isabella Mwampamba ambaye ni Balozi wa Utalii hapa Nchini kwani amechangia kiasi cha shilingi Milioni 2 ambazo alizihifadhi katika Kibubu toka mwaka 2019 kwa kushirikiana na Mumewe Mr Daniel Mwampamba huku akiwaomba wadau wengine wajitokese kuwachangia walemavu hao.
Aidha Mh. Nyamoga ametoa fedha taslimu shilingi laki tatu pamoja na kuahidi kuwapeleka magodoro walemavu hao ili yaweze kuwasaidia katika kipindi hiki ambacho balozi Isabella na wadau wengine wanaendelea kukusanya fedha za kukamilisha miradi hiyo ambayo itagharimu kiasi cha shilingi milioni 20.
Aidha Mh. Nyamoga amewataka wakazi wa kijiji cha lulanzi kushiriki kwa kutoa nguvu kazi hasa kuchimba mtaro wa kupeleka maji pamoja na shughuli za kufyatua Tofali na kuandaa mawe ya ujenzi wa nyumba na jiko la walemavu hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Mh. Peres Magiri ambaye alichangia papo hapo shilingi elfu 50, huku ofisi yake ikiahidi kutoa shilingi Milioni moja sambamba na kumpongeza Balozi Isabella kwa kuwa na moyo wa ubinadamu wa kuwakumbuka walemavu hao ambao wana uhitaji wa mkubwa wa huduma za kijamii huku serikali ya Wilaya ikiahidi kushirikiana naye kuhakikisha wanatimiza lengo waliloliweka.
Awali Diwani Kata ya Mtitu Mh. Mkakatu amemuahidi Mkuu wa Wilaya ya Iringa pamoja Mbunge wa Jimbo hilo kuwa atahakikisha anawaongoza wakazi wa kijiji cha lulanzi kushiriki kwa kufyatua matofali na kuandaa mawe yatayowezesha ujenzi wa jiko na nyumba ya kisasa kwa walemavu hao.
Mama mzazi wa walemavu hao Bi Angelista Kihanza amemshukuru Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kuwapatia fedha hizo ambazo zitawasaidia kutatua changamoto za watoto wake.
Jumla ya shilingi milioni 10 zimepatikana Katika harambee hiyo ambapo kati ya hizo, Waziri Mkuu Mh. Majaliwa ametoa kiasi cha shilingi Milioni 5, Mbunge wa Kilolo Mh. Nyamoga shilingi laki 3, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo shilingi Milioni 1, huku watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mhandisi wa Tanesco, Mhandisi wa Maji, na baadhi ya viongozi wa Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya wakitoa ahadi ya kuchangia fedha.
Hata hivyo Fedha zote zinapolokelewa kupitia acaount namba ya CRDB iliyosajiliwa kwa jina la Isabella African Foundation ya 015C621885600 huku Miradi hiyo ikitarajiwa kukamilika kwa muda wa miezi mitatu kuanzia mwezi Mei mpaka Julai 2022.