Njombe kumekucha! Maandalizi ya uzinduzi mbio za mwenge
25 March 2022, 9:11 am
Harakati za uzinduzi wa Mwenge unaotarajiwa kuzinduliwa April 2 mwaka huu katika uwanja wa Sabasaba Mkoani Njombe zimepamba moto ambapo zaidi ya watu 10,000 kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Njombe wanatarajiwa kushiriki katika shughuli hiyo ya uzinduzi ya Mwenge.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kisa Gwakisa Kasongwa amesema wiki moja kabla ya zoezi la uzinduzi huo kutakuwa na shughuli za maonyesho ya taasisi mbalimbali pamoja na wajasiliamali hivyo amewataka watu wote kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini kuhakikisha kuwa wanafika kutazama maonyesho hayo pamoja na uzinduzi.
“Tayari tumeshatenga maeneo kwaajili ya kufanya maonyesho ya taasisi mbalimbali, lakini pia wajasiliamali wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula nao tumewatengea maeneo yao”, Amesema Bi. Gwakisa.
Ameongeza kuwa imezoeleka mara nyingi shughuli za maonyesho na biashara hufanyika baada ya kuzinduliwa kwa Mwenge lakini wao wameonelea ni vyema kuanza shughuli hizo mapema kabla ya tukio la uzinduzi.
Aidha kwa upande wa Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapnduzi mkoa wa Njombe Erasto Ngole amesema hii ni fursa ya kipekee kwa wakazi wa Mkoa wa Njombe hivyo amewaasa kuitumia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi ikiwa ni ishara ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hasani kwa kuupa heshima mkoa huo kwa kufanya uzindu huo wa Mwenge.
Ameongeza kuwa uzinduzi huo utahusisha Viongozi wakuu wa kitaifa na watu wa mikoa mbalimbali hivyo wakazi wa Njombe na wilaya zake zote wanapaswa kufika kwani ndio fursa pekee ya kuwasilisha vilio vyao na kuhimiza kuanzishwa kwa miradi mbalimbali ya kiuchumi kama Liganga na Mchuchuma.
“Nitashangaa sana kuona wakuu wa nchi na watu wa mikoa mbalimbali wanafika hapa halafu wewe mtu wa Uwemba, Itulike na kwingineko mnashindwa kufika katika viwanja hivi vya Sabasaba na kushuhudia Uzinduzi” Amesema Ngole.
Emmanuel George ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Njombe ambaye pia katika shughuli ya uzinduzi wa Mwenge ni Katibu wa kamati ya Itifaki, mapokezi pamoja na Malazi amesema kamati yake imejipanga vyema kuhakikisha watu wote watakaofika katika uzinduzi huo wanapata huduma stahiki.
Amesema katika kuhakikisha kuwa kila mwananchi anayefika katika uwanja huo ili kushuhudia Uzinduzi huo anapata fursa ya kuona kinachoendelea wameandaa Televisheni ambazo zitafungwa katika maeneo mbalimbali ya kuzunguka uwanja zitakazokuwa zinaonyesha matukio yanayoendelea katika Uwanja huo.
Sanjari na hilo pia Amesema wamejipanga vyema katika kuhakikisha wageni wote watakaoingia mkoani humo wanapata huduma nzuri ya chakula na malazi.