Wananchi Wazuia Msafara Wa Waziri Wa Maji, Walia Kero Ya Maji
1 August 2022, 9:11 am
WANANCHI wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha wamezimka kuuzuia msafara wa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kulalamikia kukosa maji ya matumizi mbalimbali kwa muda mrefu.
Kufuatia hali hiyo Waziri Aweso alilazimika kuchukua maamuzi magumu ya kutangaza kuzivunja Jumuiya za Watumia Maji wa eneo hilo kwa kushindwa kutekeleza majuku vizuri.
Alichukua uamuzi huo baada ya wananchi kuzuia msafara wake wakiwa na ndoo za maji,mabango na matawi ya miti
wakitaka serikali ichukue hatua ya kutatua changamoto hiyo.
Wananchi hao walimweleza waziri kuwa kumekuwa na upendeleo wa ugawaji wa maji machache yanayopatikana kwa kuwagaiwia wafanyabiashara wenye hoteli (camp) huku wananchi wakitaabika bila maji.
Walisema Kamati za Maji ndio zimekuwa zikifanya kazi ya kupeleka maji kwa wafanyabiashara huku taasisi zikiwano shule zikinyimwa maji na kusababisha wanafunzi kushindwa hata kwenda kwenye vyoo.
Devota Martin mjumbe wa serikali ya kijiji cha Kigongoni alisema changamoto ya maji katika eneo la MtowaMbu linatokana na miundombinu ya maji kuwa midogo ambayo ilijengwa tangu mwaka 1970.
“Maji yanapelekwa kwa wenye fedha shule yetu Kigongoni hawaendi choo na hawapikiwi chakula kwasababu hakuna maji,” alisema.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akijibu malalamiko ya wananchi hao alisema serikali iliagiza Wakala wa Maji na
usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wayaanishe maeneo yote yenye changamoto.
Kufuatia hali hiyo alimwita Meneja wa RUWASA Mkoa wa Arusha, Joseph Makaidi atowe maelezo kwa wananchi juu ya hatua zilizofikiwa mpaka sasa dhidi ya changamoto ya maji eneo la Mtowambu.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Arusha,Makaidi alisema zaidi ya Sh.bilioni 1.7 zimetengwa kwa ajili ya kumaliza tatizo sugu la maji katika eneo la Mtowambu.
Alisema kinachosubiriwa kwa sasa ni kukamilisha taratibu za manunuzi na hatimaye aweze kutangazwa mzabuni atajayeanza kujenga mradi wa maji.
Waziri wa Maji, Aweso alisema serikali iliwagiza RUWASA kuainisha maeneo yote yenye changamoto ya maji ili
yaweze kupatiwa ufumbuzi.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso alilazimika kutembea kwa miguu na wananchi hao kwenda kwenye eneo ambalo wananchi hao walimweleza imefungwa barabara yakwenda zilipo oofisiya Jumuiya ya watumia maji wa eneo hilo kwa kujenga nyumba jambo ambalo limesababishana usumbufu.
Baada ya kufika katika eneo hilo na kujionea hali halisi Aweso alipimpigia simu Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa ambaye alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Monduli Frank Mwaisumbe ambaye alikuwepo eneo hilo kulishughulikia jambo hilo kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Kufuatia hatua hiyo wananchi walilipuka kwa shangwe na kuelezea kuwa hapa nchiniwanatakiwa viongozi kama Aweso ambae anatatua migogoro kwa wakati kwa kuwasiliana na wahusika wengine moja kwa moja.