Wizara ya Afya yaagiza Sikoseli kupimwa vituo ngazi ya msingi
19 June 2022, 4:47 pm
Serikali imeingiza ugonjwa wa Sikoseli kwenye mpango mkakati wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na kuhakikisha huduma za vipimo na matibabu zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi.
Hayo yamesemwa leo Juni 19 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe wakati wa maadhimisho ya siku ya sikoseli duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Arusha.
Dkt. Shekalaghe amesema Serikali itaanzisha kliniki za sikoseli katika Hospitali za wilaya, mikoa, Kanda na taifa ili wagonjwa wasisafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
“Tunaweka mikakati Wizarani kuwa mwaka ujao wakati tunaadhimisha siku hii tutahakikisha changamoto ya kutafuta huduma umbali mrefu inakua haipo kwani kliniki za Sikoseli zitakua karibu na wananchi lakini pia NHIF kuhakikisha kuwa katika vile vitita huduma hizi zinaingizwa katika bima ya Afya ili waweze kupata huduma hii vizuri kwa sababu huu ni ugonjwa ambao watu wanaishi nao maisha yao yote,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Dkt. Shekalaghe ameongeza kuwa Tanzania ni nchi ya tano Duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye Sikoseli ambapo kila mwaka wanazaliwa watoto 11,000 na mpaka Sasa idadi ya watu wenye sikoseli ni 200,000 ambapo watu 5 mpaka 7 kati ya 100 waliopo chini ya miaka mitano hufariki kwa sababu mbalimbali kutokana na madhara yanayosababishwa na Sikoseli.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Silvia Mamkwe ameitaka jamii kuondoa mila potofu juu ya ugonjwa wa Sikoseli badala yake wazingatie kufanya vipimo wakati wa kupata wenza ili kuepuka kuoana wote wakiwa na vinasaba vya Sikoseli vinavyofanana hali itakayosaidia kutozaa watoto wenye ugonjwa huo.
Mmoja wa mashujaa wa Sikoseli ambaye ameishi na ugonjwa huo kwa miaka 44 Sanyu Singa amesema wao kama mashujaa wanakabiliwa na changamoto nyingi lakini kubwa ni elimu juu ya Sikoseli kutokuwepo katika jamii.