TFRA yawanoa wakulima, Amcos na wafanyabiashara Iringa
21 October 2024, 12:58 pm
Na Adelphina Kutika
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Nyanda za Juu Kusini imejizatiti kuwajengea uwezo wakulima na mawakala wa mbolea ya ruzuku mkoani Iringa ili kuboresha utendaji wao.
Wakizungumza mara baada ya mafunzo yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili katika Kituo cha Watu Wenye Mahitaji Maalum Neema Craft, Manispaa ya Iringa mkoani Iringa, washiriki wamesema elimu waliyoipata kuhusu matumizi sahihi ya mbolea itasaidia kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa mazao.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondia, amesema kuwa mkakati wao ni kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ili kuimarisha uwezo wa wakulima na mawakala.
Naye Marry Raymond Mlayi, mkufunzi kutoka Chuo cha Kilimo Uyole, ameongeza kuwa mafunzo hayo yalijumuisha wafanyabiashara, washiriki kutoka AMCOS, na wakulima, yakiwa na lengo la kuboresha afya ya udongo na kukabiliana na changamoto za kilimo.
Kwa upande wake Afisa Kilimo ambaye pia ni Mkaguzi wa Pembejeo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Daudi Amos Chilagani, ameshukuru serikali kupitia mamlaka ya udhibiti mbolea kwa kutoa mafunzo hayo kwa wauzaji, akisema kuwa watakuwa msaada mkubwa kwa wakulima wanapohitaji elimu ya matumizi ya pembejeo kuelekea msimu wa kilimo.
Katika kuimarisha uwezo wa wakulima na mawakala, Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea (TFRA) inachangia katika kuhakikisha usalama wa chakula na ukuaji wa sekta ya kilimo katika mkoa wa Iringa.
MWISHO