Mbunge Lupembe aishukuru serikali kwa fedha za madarasa na Vyoo Jimbo la Nsimbo
14 April 2023, 7:20 pm
Fedha hizo zitasaidia kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jamii.
Na Halfan Akida
Mbunge wa jimbo la Nsimbo, Mh Anna Lupembe ameishukuru serikali kwa kutoa bilioni 6.2 kwa ajili ya miradi ya maendeleo Nsimbo, mkoani katavi.
Lupembe amesema hayo leo bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia katika bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali na Mitaa (TAMISEMI).
Ameshukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kujenga madarasa na vyoo katika shule shikizi zilizopo mkoani Katavi hususani katika jimbo la Nsimbo.
Lupembe ameishauri serikali kuhakikisha wanawajengea walimu wa vijijini nyumba kwa ajili ya makazi ili kuwapa moyo wa kuendelea kufanya kazi katika mazingira hayo.
Aidha Lupembe ameiomba serikali kumalizia fedha za ujenzi wa vituo vya afya Ugala na Itenka ambao tayari serikali imeshatoa shilingi milioni 500 kwa kila kituo kati ya milioni 800 zilizoahidiwa kwa kila kituo.
Katika hatua nyingine Mbunge Anna Lupembe ameiomba serikali kuwapatia posho wenyeviti wa vijiji kutokana na kazi kubwa wanazozifanya za kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo majimboni.
Mbunge huyo wa Nsimbo pia ameipongeza Tarura nchini kwa namna wanavyofanya kazi ya kuhakikisha barabara zinapitika katika vipindi vyote na kusaidia wananchi hususani wakulima kuendelea kuuza mazao yao shambani.
Pia Lupembe ameiomba serikali kuiongezea fedha Tarura kutokana na mtandao mkubwa wa barabara walio nao hususani za vijijini zinazoharibiwa sana na mvua katika kipindi hiki.