Bilioni 1 kuweka Taa za Barabarani 180 Mafinga Mkoani Iringa
6 April 2023, 10:53 am
Mradi huo unagharamiwa kwa pamoja kati ya halmashauri ya mji huo na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) watakaochangia Sh Milioni 500 kila mmoja.
Na Frank Leonard
KIASI cha Sh Bilioni moja kinatarajiwa kutumika kuweka taa 180 za barabarani zitakazotandazwa kwa umbali wa kilometa tano katika mji wa Mafinga, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Mkataba wa mradi huo utakatekelezwa kwa siku 120, umesainiwa mjini Dodoma leo kati ya Mkurugenzi wa REA Mhandisi Hassan Saidy kwa upande mmoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Happiness Laizer kwa upande wa halmashauri katika hafla iliyohudhuriwa na Mwenyekiti wa Mji Mafinga, Regnant Kivinge.
Wengine waliokuwepo ni pamoja na Wakili wa Serikali, Gasper Kalinga, Mwanasheria wa REA Mussa Muze, Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi na Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia, Mhadisi Advera Mwijage.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga alisema mradi utachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika mji wake, kwani utawawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao hadi nyakati za usiku kwa uhuru na usalama.
Naye Mbunge wa Mafinga Mjini, alisema ni fahari sana kwa wananchi wa mji Mafinga kupata mradi huo waliouomba kwa muda mrefu, ili uwanufaishe kwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na usalama wao nyakati za usiku.
“Lakini pia taa hizo zitaung’arisha na kuupendezesha mji wa Mafinga kwa kuuongezea muonekano mzuri wakati wa usiku,” alisema Kivinge.
“Wananchi wa Mafinga wamekuwa wakisubiri mradi huu kwa shauku sana, sasa wafanyabiashara wakae mkao wa kufanya biashara zao kwa saa 24; mradi utakapokamilika ni wajibu wetu kuutunza,” alisema Chumi.
Akitoa takwimu za Mradi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, alisema utatekelezwa kwa siku 120 na akataja maeneo yatakayoguswa kuwa ni pamoja na Kinyanambo A,B na C, Mafinga Hospitali, CF plazer- tanki la maji.
NSSF- Bomani, Luganga- Mgololo, Mashujaa-Royal Park Hotel, Chaibora- Dembe, na NMB-mashujaa-Mashine ya mpunga.
Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake zinazolenga kuboresha upatikanaji matumizi ya nishati ya umeme mijini na vijijini.