Madiwani Iringa waomba kondomu
28 February 2024, 9:37 am
Na Hafidh Ally
Ongezeko la uzalishaji wa pombe ya kienyeji aina ya ulanzi na mahusiano yake na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) limewaibua baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Iringa wakitaka usambazaji wa kondomu katika vilabu vinavyouza pombe hiyo kuongezwa.
Madiwani hao wameiomba kamati ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi kuhakisha mipira hiyo ya kiume haikosekani katika maeneo hayo na mengine yote hatarishi.
“Ulanzi ni moja ya kilevi ambacho tafiti mbalimbali zinaonesha kimekuwa kichocheo cha ngono zisizo salama na matokeo yake ni ongezeko la maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya ngono. ” alisema mmoja wa madiwani hao, Vumilia Mwenda.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani lililofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Ihemi, Mwenda alisema kuna ongezeko kubwa la uzalishaji wa pombe hiyo katika kipindi hiki cha mvua za masika.
Pombe hiyo iliyogunduliwa wakati wa utawala wa machifu wa kabila la Wabena katika Wilaya ya Njombe baada ya mti mchanga wa mwanzi kukatika na kuanza kutoa maji matamu, imekuwa ikithaminiwa na wakazi wa mkoa wa Iringa na tangu wakati huo, imesambaa na kufika katika maeneo mengine mengi hasa kusini mwa Tanzania.
Akipigilia nyundo hoja hiyo Diwani wa Kata ya Maboga, Venny Myinga alieleza kwa mifano jinsi hali ya maambukizi ya VVU ilivyo mbaya katika maeneo ya vijijini na kuomba maeneo hayo yatazamwe kwa jicho la tatu.
“Hakuna ubishi kwamba maambukizi ya VVU katika maeneo mengi ya vijijini yamekuwa yakisababishwa na tabia ya ulevi ambao moja ya sifa yake ni kuifanya ngono kuwa rafiki yake,” alisema.
Akizungumzia upatikanaji wa pombe hiyo na gharama yake ndogo, Myinga alisema; ” Unywaji wa pombe unaweza kuongeza hatari ya maambukizi kwa kuathiri maamuzi na tabia, kama vile kutozingatia matumizi sahihi ya kinga wakati wa kujamiiana.”
Myinga alisema watu wanaoshiriki vitendo vya ngono bila kinga wanaweza kuwa katika hatari zaidi wanapokuwa chini ya ushawishi wa pombe hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari na kufahamu hatari zinazoweza kutokea katika mazingira hayo.
Akijibu hoja hizo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Saumu Kweka alisema kusambaza kondomu katika maeneo ya starehe ni muhimu katika mikakati ya kitaifa ya kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa na kudhibiti mimba zisizotarajiwa.
Kweka alisema mkakati huo unaweza kuchangia afya bora na kupunguza mzigo wa matatizo ya kiafya na kijamii.
Hata hivyo alisema halmashauri yao inatekeleza kwa vitendo ombi la madiwani hao kwa kuweka kondomu katika maeneo mengi ya umma ikiwamo Bar, vilabu, masokoni, na nyumba za kulala wageni.
“Maeneo yote hatarishi tunayafikia na tumekuwa tukifanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha yana mipira hiyo ya kiume na kazi inaendelea,” alisema.
Kwa mujibu wa takwimu ya utafiti wa hali ya Maambukizi ya Ukimwi nchini iliyofanyika kati ya mwaka 2016 na 2017, mkoa wa Iringa Mkoa wa Iringa ni wa pili kitaifa ukiwa na asilimia 11.3 ya maambukizi hayo huku maambukizi katika halmashauri hiyo ya Iringa yakiwa kwa asilimia 5.7.