Iringa kupanda miti milion 42 kutunza mazingira
16 January 2025, 12:46 pm
Na Joyce Buganda
Serikali ya mkoa wa Iringa inatarajia kupanda zaidi ya miti millioni 42 kwa kipindi Cha mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi za serikali ya awamu ya 6 Ili kutunza mazingira.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya kilolo Joachim Nyingo ambae alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba wakati wa uzinduzi wa ugawaji na upandaji wa miti yaliyofanyika kimkoa Wilaya ya kilolo katika shule ya Sekondari ya Wasichana Lugalo iliyopo wilayani kilolo na kusema miti hiyo ikitunzwa itakuja kusaidia vizazi na vizazi.
Dc Nyingo amesema miti iliopandwa shuleni hapo anatamani itunzwe vizuri Ili ije kuleta manufaa kwa watakaokuepo wakati huo lakini kwa sasa jukumu la kuitunza ni kwa hao waliopo.
Aidha Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Isaak Mgovano amesema kwa msimu wa mwaka 2023/2024 mkoa wa Iringa ulioanda miti 42,132,403 ambapo tathmini ya miti iliopo bado inaendelea kufanyika.
Mgovano amesema changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni moro kichaa ambayo husababisha hasara kubwa, uhaba wa mbegu bora za muda mfupi pia baadhi ya maeneo miti huharibiwa na mifugo.
Kwa upande wake Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Kilolo Essau Muhonda amesema ugawaji wa Miche kwa wananchi na wadau Huwa ni bure hivyo ni vyema kuitunza.
Ameongeza na kusema kwa kipindi Cha mwaka 2023/2024 TFS mkoa wa Iringa imezalisha zaidi ya miche Milioni 8 katika bustani zao zilizopo Wilaya ya kilolo, Iringa pamoja na shamba la miti la Sao hill ambayo ni kwajili ya matumizi mbalimbali kama matunda, vivuli, na miti ya kuhifadhi vyanzo vya maji.
Ikumbukwe uzinduzi wa upandaji na ugawaji wa Miche kitaifa hufanyika mwezi Aprili lakini mkoa wa Iringa hufanyika Kila mwaka tarehe januari 15 kutokana na Hali ya hewa ya mkoa wa Iringa ilivyo.