USAID yapongezwa kwa kuwezesha vijana na wanawake Iringa
12 January 2025, 11:17 am
Na Godfrey Mengele
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Komred Kheri James ameipongeza USAID Tanzania kupitia Mradi wa Feed the Future Tanzania imarisha Sekta binafsi, pamoja na wadau wao Agriedo Hub kwa kuwezesha vikundi vya vijana na Wanawake wilayani humo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya uzalishaji mali kwa vijana, Komred Kheri James ameeleza kuwa Mradi wa feed the future unaofadhiliwa na USAID Tanzania umewezesha vijana zaidi ya 700 kwa namna mbalimbali ikiwemo mafunzo, Mitaji, Vifaa, Masoko ya bidhaa kuwaunganisha vijana na Taasisi za fedha na kuwagawia nyezo za kuongeza uzalishaji na tija katika shughuli zao.
Aidha Komred Kheri James amewapongeza vijana 75 kati ya 100 waliokabidhiwa vitendea kazi na amewasihi kuvitunza na kuvitumia vyema ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao.
Pamoja na mambo mengine Komred Kheri James amezipongeza Taasisi zote zinazofanya kazi ya kuwajengea uwezo vijana wilayani Iringa, na amewahakikishia vijana na wadau wa maendeleo kuwa Serikali itandelea kuwajibika na kutoa ushirikiano kwa wadau wote ili kuendelea kuwajenga na kuwainua vijana wa Tanzania.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Iringa, Wadau kutoka mashirika mbalimbali na maafisa kilimo kutoka katika Halmashauri za mkoa wa Iringa.