Iringa yajipanga kupandisha ufaulu
12 January 2025, 11:04 am
Na Adelphina Kutika
Mkuu wa wilaya ya Iringa Komred Kheri James amewataka wadau wa elimu wilayani Iringa kujipanga kikamilifu ili kupandisha ufaulu na kusimamia malezi na maadili ya watoto.
Komred Kheri James ameyasema hayo katika kikao kazi cha Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari kilichokua na lengo la kuweka mikakati bora ya kuanza mwaka wa masomo na kutoa maelekezo ya Serikali katika maandalizi ya ufunguzi wa shule mapema wiki ijayo.
Akizungumza katika kikao hicho Komred Kheri James ameeleza kuwa wilaya ya Iringa imebarikiwa watoto wenye akili, Walimu wenye uwezo na Serikali imeendelea kuboresha mazingira bora ya utoaji wa elimu, hivyo kuna kila sababu ya kupandisha ufaulu wa watoto katika mitihani yote ya ndani na nje.
Aidha kupitia kikao hicho Mheshimiwa Mkuu wa wilaya amewapongeza Wakuu wa shule na walimu wote wa wilaya ya Iringa kwa kazi kubwa walio ifanya ya kitaaluma, malezi, Usimamizi wa miradi na ushirikiano mkubwa kwa jamii.
Kipekee Komred Kheri James amehimiza uwajibikaji, Ubunifu, ushirikiano na usimizi madhubuti wa mipango na maamuzi yanayo gusa ustawi wa elimu.
Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya amewahimiza wazazi kuwapeleka watoto shule mara tu zitakapofunguliwa na kuhakikisha wanaweka misingi bora ya kushirikiana na walimu ili kuongeza Usimamizi wa watoto kimalezi na kitaaluma.
Kikao kazi hicho kilihudhuriwa pia na Kamati ya Usalama ya wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa elimu, Maafsa Tarafa na wakuu wote wa shule za Msingi na Sekondari katika Wilaya ya Iringa.