DC Kheri apongeza usimamizi wa miradi ya elimu Iringa
25 November 2024, 10:01 am
Na Adelphina Kutika
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, amewapongeza wakuu wa shule kwa usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, akieleza kuwa wameonyesha uaminifu mkubwa katika kusimamia miradi hiyo.
Haya yamejiri katika kikao cha uzinduzi wa jukwaa la mafanikio, kilichohusisha wakuu wa shule, wanazuoni na Tanesco, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa.
Mkuu wa Wilaya alieleza kuwa fedha zote zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hazijashuhudia taarifa yoyote ya ubadhilifu mpaka miradi hiyo inakamilika, akionyesha kuridhika na jinsi ambavyo miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.
Afisa Elimu ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Peter Fussi, alitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, akisema kuwa katika fedha zilizotengwa kwa ajili ya miundombinu ya elimu, mafanikio makubwa yamepatikana.
Aidha, baadhi ya wanazuoni kutoka vyuo mbalimbali mkoani Iringa, waliohudhuria jukwaa hilo, wamepongeza kamati tendaji ya Mkuu wa Wilaya kwa juhudi zao katika kufanikisha maendeleo ya wilaya ya Iringa, wakieleza kuwa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali umesaidia katika utekelezaji wa miradi hiyo.
MWISHO