DC Linda awaonya wanaowatumia walemavu kitega uchumi
29 April 2024, 9:55 am
Vitendo vya udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu ikiwemo suala la kuwatumia kujinufaisha kiuchumi limeonekana kushamiri wilaya ya Mufindi.
Na Hafidh Ally
Wananchi wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wametakiwa kujenga utaratibu wa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum kuliko kuwafanya vitega uchumi kwa kuwatembeza barabarani ili waombe misaada.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt Linda Salekwa Katika hafla ya chakula cha pamoja na watu wenye uhitaji maalumu sanjari na utoaji wa misaada mbali mbali kwa wahitaji hao hafla iliyoandaliwa na kanisa la Waadiventista Wasabato-Mafinga na kuongeza kuwa kufanya hivyo ni udhalilishaji dhidi ya kundi hilo.
Dkt Salekwa ameishukuru serikali kwa kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi na watu wenye ulemavu kupata vifaa mbalimbali na maiundombinu ya elimu rafiki kwao.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi Doroth Kobelo amesema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wenye uhitaji maalumu hivyo jamii imeaswa pia kuendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalumu kupata huduma stahiki.
Naye Mch.Philibert Mwanga Mkurugenzi wa Huduma Wezeshi amesema kanisa linapaswa kuwa mfano mzuri wa kuwasaidia wenye mahitaji maalumu hivyo kwa kutambua hilo darasa la watu wanaotumia alama litafunguliwa na wale wenye kuhitaji kujifunza.
MWISHO