Ng’ombe 547 wakamatwa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha
28 March 2024, 12:51 pm
Wahifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Mkoani Iringa wameeleza kukaniliana na changamoto kwa wanaochunga mifugo yao hifadhini.
Na Mwandishi wetu
Ng’ombe 547 wamekamatwa wakichungwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kinyume cha sheria, huku wachungaji wakikimbia na kuitelekeza mifugo hiyo.
Hifadhi hiyo ni kati ya maeneo ambayo yamekuwa yakiharibiwa na kusababisha madhara ya kimazingira, ikiwemo kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Godwell Meng’ataki amesema ilikamatwa eneo la Ukwaheri ndani ya bonde lenye ardhi oevu la Usangu.
Amesema wamekuwa wakiendelea kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira, hususani katika bonde hilo lenye vyanzo muhimu vya maji kwa ajili ya mto Ruaha Mkuu na bioanuai muhimu kwa mazingira, uhifadhi na utalii.
Amesema Mahakama imeshatoa amri mifugo hiyo itaifishwe na imeshateua dalali wa kuiuza.
Ameeleza jitihada za uhifadhi katika bonde hilo zitaendelea kwa nguvu zote, ikiwemo kupitia doria za miguu, anga, magari na kushirikiana na wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Mkuu wa Kanda ya Usangu, Mhifadhi daraja la pili Abisai Nassari, ametaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ni maeneo ambayo mifugo inawekwa ikishaingizwa katika hifadhi kuwa magumu kufikika.
Amesema mifugo huingizwa katikati ya matindiga, inakuwa vigumu kwa askari kufika hivyo kulazimika kushirikiana na kikosi cha anga kuyafikia na kusogeza mifugo kwenye maeneo mengine ambayo askari wanaweza kufika.