Nyumba ya watu wenye ulemavu Lulanzi Mkoani Iringa yawekwa milango madirisha na kupigwa plasta
4 July 2022, 4:19 pm
Nyumba inayojengwa kwa familia ya watu watatu wenye ulemavu katika kijiji cha Lulanzi Kilichopo Kata ya Mititu Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa imefikia hatua ya kupigwa plasta, kuwekwa milango na madirisha.
Akizungumza na Nuru fm kuhusu maendeleo ya ujenzi huo, Balozi wa Utalii Isabella Mwampamba ambaye anaratibu zoezi la mradi huo wa ujenzi, amesema kuwa kwa sasa nyumba hiyo imefikia hatua hiyo kutokana na michango ambayo amekuwa akiipokea kutoka kwa wadau wa maendeleo kupitia taasisi yake ya Isabella African Foundation.
Amesema kuwa kwa sasa mafundi wanaendelea na ujenzi ila bado kuna uhitaji wa vifaa vya ujenzi kama vile Simenti, mchanga na vifaa vya kumalizia zoezi hilo ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na ushirikiano wa serikali ya Wilaya ya Kilolo kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Ofisi ya Kaimu katibu tawala wilaya ya kilolo pamoja na ushirikiano kutoka kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. MAJALIWA KASSIM MAJALIWA.
Hata hivyo Balozi Isabella amesema kuwa anatarajia kupokea msaada wa baadhi ya vifaa vya maji na Umeme kutoka Taasisi ya Bulk Distributors kutoka Arusha ili kukamilisha ujenzi wa nyumba ya watu hao watatu wenye ulemavu.
Katika Hatua Nyingine Isabella amewaomba wadau wa maendeleo kuendelea kutoa michango kwa kuwasiliana naye kupitia namba 0762 756046 ili waweze kupewa utaratibu wa kuoa michango yao au kutuma moja kwa moja kupita acaount namba ya CRDB iliyosajiliwa kwa jina la Isabella African Foundation ya 015C621885600.
Kwa upande wake mama mzazi wa walemavu hao Anjelista Kihanza amemshukuru balozi wa utalii Nchini Isabella mwampamba pamoja na serikali kwa ujumla kwa kuwasaidia kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili huku wakifurahia uwepo wa nyumba hiyo ya kisasa ambayo inatajaria kukamilika hivi karibuni.