Ugonjwa wa Monkeypox ‘wabisha’ hodi Nchini Uganda
11 June 2022, 8:13 am
Taasisi ya Utafiti wa Virusi nchini Uganda (UVRI), imetangaza kuwaweka katika uangalizi maalumu watu sita, wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa wa Monkeypox.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Prof. Pantiano Kaleebu, amesema sampuli zilizochukuliwa kwa watu hao zimesafirishwa nchini Afrika ya Kusini kufanyiwa uchunguzi, kutokana na Uganda kutokosa vifaa vya kupimia ugonjwa huo.
“Hatuna vifaa vya upimaji imebidi kupeleka sampuli Afrika ya kusini na wagonjwa hawa ni wakimbizi wawili wa Kikongo wenye umri wa miaka 2 na wanne wenye miaka 12,” alisema Prof. Kaleebu.
Amesema taasisi ya UVRI ilianza uchunguzi wa awali, baada ya kupata taarifa kuwa watu sita walionesha dalili zinazofanana na zile zinazotajwa kusababishwa na maradhi yatokanayo na nyani, yaani Monkeypox.
“Tunashuku muingiliano wa watu mpakani mwa DRC na Uganda umesababisha maambukizi ya ugonjwa huu na upo uwezekano wa kusambaa kwa haraka maeneo mengine,” alifafanua msemaji huyo.
Prof. Kaleebu amesema kesi mbili kati ya zinazoshukiwa zipo katika Wilaya ya Kisoro kusini magharibi mwa Uganda, eneo ambalo linapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda, huku wagonjwa wanne wakiwa katika Jiji la Kampala.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema kuna hatari ya ugonjwa huu kusambaa kwa haraka, kwani tayari umeathiri baadhi ya watu wa Mataifa mengi hasa barani Ulaya.