Askari polisi Iringa asakwa kwa tuhuma za mauaji
16 December 2024, 10:27 am
Na Ayoub Sanga
Jeshi Polisi Mkoa wa Iringa linawatafuta Askari namba F. 4987 Sajenti Rogers Joshua Mmari wa kituo cha Polisi Ipogolo na Askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo) Thomas Mkembela kwa tuhuma za kumuua Nashon Kiyeyeu (23) Mkazi wa Nyamhanga kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa SACP, Allan L. Bukumbi amesema kuwa chanzo cha mauaji hayo inadaiwa kuwa mnamo Tarehe 14 Disemba 2024 Sajenti Rogers alipokea taarifa kutoka kwa Mwanachi mmoja ambaye hakumtaja Jina kuwa anamtuhumu Nashon Kiyeyeu kuwa ameibiwa simu yake ndipo waliposhirikiana kumkata na kumpiga hadi kupelekea umauti.
Kamanda Bukumbi amesema kuwa Askari Thomas hawakupeleka shauri hilo katika kituo cha polisi na badala yake walifanya kazi kinyume na utaratibu na jeshi linaendelea kuwasaka ili wachukuliwe hatua za kisheria.
“Jeshi Polisi Mkoa wa Iringa linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa hao na kusambaza taarifa mikoa mbalimbali” amesema SACP, ndc Bukumbi.
Aidha jeshi la Polisi limetoa wito kwa yeyote atakayemwona Sajenti Rogers na Mgambo aitwaye Thomas Mkembela popote pale asisite kutoa taarifa ili wakamatwe na hatua zingine za kisheria zifuate.