Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia yazinduliwa Iringa
11 December 2024, 9:59 pm
Na Hafidh Ally
Wananchi Mkoani Iringa wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyozinduliwa rasmi katika Viwanja vya Mwembetogwa Mkoani Iringa.
Akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni hiyo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa iringa, amesema kuwa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inalenga kuhakikisha wananchi wanapata haki bila gharama yoyote.
Mh. Ngwada amesema kuwa kampeni hiyo itasaidia wananchi kujua haki za wanawake na watoto,kuwashauri manusura wa ukatili wa kijiji sambamba na kutatua migogoro katika maeneo ya kijamii.
Naye Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi CCM mkoa wa Iringa Joseph Ryata ameishukuru serikali kwa kuja na kampeni ya Msaada wa kisheria kwani itasaidia wananchi kupata haki kwa muda muafaka.
Kampeni hiyo ya Mama Samia inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu ndani ya jamii ikiwemo haki za wanawake na watoto, huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia Pamoja na kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu wajibu na misingi ya utawala bora.
MWISHO