RC Serukamba agoma kukagua miradi
23 April 2024, 10:12 am
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba ameagiza kufanyika ukaguzi wa miradi ambayo haitekelezwi na kujua changamoto inayokwamisha utekezaji wake.
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amekataa kuendelea na ziara ya kukagua miradi isiyo na changamoto aliyopangiwa na kutaka apelekwe kwenye miradi kiporo iliyokwama kutekelezwa kwa muda mrefu.
Mkuu huyo wa mkoa ambaye jana alipanga kuanza ziara yake katika kata za Ihemi na Ifunda alisitisha ziara yake majira ya saa 6 mchana baada ya kufika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini mara baada ya kukabidhiwa taarifa ya miradi atakayokagua kwenye ziara hiyo.
Baada ya Kaimu Mkurugenzi kutambulisha watumishi waliokuwepo kwenye ukumbi huo wa halmashauri huku akimkaribisha msoma taarifa kusoma taarifa hiyo mbele ya mkuu huyo wa mkoa ghafla Serukamba alisimamisha zoezi hilo na kutaka kupewa idadi ya miradi yote inayotekelezwa katika halmashauri hiyo hali iliyopelekea zoezi la usomaji taarifa kusimama kwa muda wa takribani dakika 10 hivi wakati taarifa ya miradi hiyo ikifuatwa na baada ya kuletwa taarifa hiyo ya miradi alitaka kaimu mkurugenzi aoneshe miradi ambayo amepangiwa kukagua kama kwenye orodha ya miradi kiporo ya halmashauri hiyo ipo.
“Sasa hii miradi ambayo leo mnanipeleka ni miradi ipi kama kwenye orodha ya miradi yote kiporo ya halmashauri haipo mlitaka kuniingiza chaka wakati nilitoa maelekezo kuwa ziara yangu itaangazia miradi kiporo yote ambayo serikali ilikwishatoa pesa na haijakamilika “alisema Serukamba.
Ameongeza kuwa hawezi kuendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi mizuri ambayo amepangiwa kwenye ratiba wala kwenda kufanya mkutano wa hadhara kijiji cha Ifunda kama hajatembelea miradi yote kiporo ambayo serikali ilikwishatoa pesa .
“Mimi sipo hivyo si kiongozi wa kukubali kudanganywa kirahisi hivi hii miradi mnayotaka kunipeleka ni miradi ambayo hakuna mafundi wanaoendelea na kazi nitakwenda kumuuliza nani huku na miradi mingi hapa mmenichagulia mizuri isiyo na dosari Mimi nataka miradi yenye changamoto ili nijue shida ni nini na serikali ilikwisha toa pesa za kukamilisha miradi hiyo “
Hivyo aliagiza kusitishwa kwa ziara hiyo kwa Siku ya Jana ili maofisa hao wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Vijijini kukaa kuchambua miradi yote kwa Kanda ama tarafa au kata ili aweze kufika kukagua miradi hiyo na miradi ambayo watampeleka ni lazima Wao wenyewe wawe walikwisha itembelea .
Mkuu huyo wa mkoa wa Iringa amepanga kuendelea na ziara hiyo jumanne baada ya jumatatu kukataa kuendelea na ziara kwenye miradi mizuri iliyochaguliwa .
Hivi karibuni kwenye kikao cha mkuu huyo wa mkoa na watumushi wa halmashauri hiyo na madiwani baadhi ya madiwani walidokeza matumizi mabaya ya fedha za miradi kwenye halmashauri hiyo na kuwa miradi mingi imekwama kutokana na matumizi mabaya ya fedha .