Mbolea ya ruzuku yamweka matatani mfanyabiashara Iringa
6 July 2023, 10:39 am
Na Frank Leornad
SERIKALI ya Mkoa wa Iringa imemnasa mfanyabiashara Maneno Yusuph Kivembele (50) mkazi wa Ilula wilayani Kilolo akihususishwa na tuhuma ya ununuzi wa mbolea ya ruzuku kwa njia ya udanganyifu na kuuza kwa wakulima kwa bei ya juu kinyume na mpango wa serikali.
Taarifa ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego aliyesema serikali inaendelea kuwasaka watu wengine wanaojihusisha na hujuma hiyo.
Wakati akikamatwa hivi karibuni alisema mtuhumiwa huyo alikuwa amekwishanunua mifuko 627 ya aina mbalimbali ya mbolea kutoka kwa mawakala na makampuni tofauti ya mbolea wilayani Iringa na Kilolo.
“Tumemkamata kwa makosa kadhaa yakiwemo ya kuuza mbolea yenye ruzuku kwa wakulima kwa bei ya kati ya Sh 82,000 na Sh 87,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50 kinyume na taratibu,” alisema.
Makosa mengine ni pamoja na kuuza mbolea bila leseni na kununua mbolea kwa kutumia vitambulisho vya wakulima wengine kinyume na utaratibu wa serikali katika usambazaji wa mbolea yenye ruzuku.
“Baada ya kupata taarifa zake na kuwekewa mtego alinaswa na kufikishwa kituo cha polisi cha Lugalo wilayani Kilolo anakoendelea kushikiliwa hadi sasa,” alisema.
Akizungumzia jinsi mtuhumiwa huyo alivyofanya udanganyifu huo, Mkuu wa Mkoa alisema katika manunuzi yake mtuhumiwa alinunua mbolea kutoka kampuni ya ETG Inputs Limited kwa kutumia namba ya mkulima 81140702890 ambayo iliandikishwa katika mfumo wa ruzuku kwa jina la Sudiana J . Mwakalinga wa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Baada ya kufuatilia usajili wa mkulima kwenye mfumo ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo alifanya udanganyifu wakati wa kujiandikisha na kujipatia namba tatu za ruzuku ambazo ni 84050311708 kwa ajili ya ekari saba, namba 84050327582 kwa ajili ya ekari 80 na namba 84050328057 kwa ajili ya ekari 120 zote zikiwa ni za kijiji cha Ilula sokoni wilayani Kilolo .
“Taarifa zote hizo zilikuwa za uongo na kinyume na utaratibu unaotaka mkulima kujisajili mara moja kwenye kijiji husika,” alisema.
Kwa upande wake Michael Sanga ambaye ni Meneja wa Kanda wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania Kanda ya Nyanda za Juu kusini alisema mtuhumiwa amekamatwa ikiwa ni matokeo ya ofisi yake na ofisi ya mkuu wa mkoa katika kudhibiti udanganyifu katika mbolea hiyo ya ruzuku.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kwamba wanaendelea uchunguzi zaidi wa suala hilo linalohisiwa kuhusisha mtu zaidi ya mmoja kabla ya mtuhumiwa huyo hajafikishwa mahakamani.