Kijana ahukumiwa kunyongwa hadi kufa Mufindi
28 March 2023, 12:17 pm
Liston Dugange mkazi wa Kijiji cha Mtambula Wilayani Mufindi ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya kukusudia dhidi ya Emmanuel Mbigi.
Na Mwandishi wetu
Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyoketi Wilayani Mufindi imetoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa Liston Dugange mwenye umri wa miaka 33 mkazi wa Kijiji cha Mtambula Wilayani Mufindi kwa mauaji ya kukusudia dhidi ya Emmanuel Mbigi mwenye umri wa miaka 19 aliyekuwa anafanya kazi ya kuchunga ng’ombe katika kijiji hicho huku mtuhumiwa mwingine aliyeshtakiwa kwa kosa hilo akiachiwa huru baada ya mahakama hiyo kutomkuta na hatia.
Liston Dugange alitenda kosa hilo mnamo tarehe 4/6/2019 majira ya saa 6 za mchana huko kijijini kwao Mtambula baada ya ya kuiba ng’ombe wawili na kumuuliza marehemu kama anamfahamu ambapo marehemu alikiri kumtambua na ndipo alipompiga na kitu kizito kichwani kisha kumkata sikio na baada ya kugundua kuwa amekufa aliutupa mwili wa marehemu kichakani.
Listoni Dugange alikamatwa tarehe 5/6/2019 katika Kijiji cha Igowole alipokuwa akitaka kuuza ngo’ombe kwa bwana Abili Mayemba ambapo mtego uliwekwa baina ya Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mtambula pamoja na Mayemba baada ya Mayemba kushtukia kuwa huenda ng’ombe hao wangekuwa wa wizi kutokana na Liston Dugange kugomea kwenda kuandikishana kwa afisa huyo.
Baada ya mtego huo Listoni alifika kijijini Igowole kwa ajili ya kufanya biashara ya ng’ombe hao ndipo alipokamatwa
Listoni alipofikishwa Mahakamani alikana kutenda kosa hilo ndipo upande wa mashtaka ukalazimika kuleta mashahidi watano kwa ajili ya kuthibitisha shtaka hilo la mauaji na ndipo mtuhumiwa alipokutwa na hatia ya kutenda kosa hilo kwa kukusudia.
Shauri hilo la mauaji namba 10 la mwaka 2019 limesimamiwa na Wakili wa Serikali Yahaya Misango ambapo aliiomba mahakama hiyo kuzingatia kifungu namba 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 rejeo la mwaka 2022 adhabu inayomtaka mshtakiwa kunyongwa hadi kufa
Kwa upande wa utetezi wa mtuhumiwa ukiongozwa na Wakili Cosmas Kishamawe aliieleza mahakama kuwa kwa kuwa mteja wake amekutwa na hatia ya kutenda kosa hilo na kosa hilo halina adhabu mbadala hivyo kwa upande wao hawana maombi juu ya shauri hilo.