INEC yasisitiza uwazi katika uboreshaji daftari la mpiga kura
19 December 2024, 9:01 am
Na Hafidh Ally
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeeleza kuwa uwepo wa mawakala kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura ni kielelezo cha uwazi na haki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo kwa watendaji ngazi ya mkoa kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Iringa, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk amesema kuwa katika kuhakikisha zoezi hilo linakuwa la uwazi, Tume imetoa kibali cha kutoa elimu kwa wapiga kura kupitia asasi za kiraia 157 na asasi zisizo za kiraia 33 kwa ajili ya uangalizi wa zoezi hilo.
Amesema kuwa watendaji hao watakuwa na jukumu la kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ili kufanikisha uboreshaji wa daftari kwa kutumia mifumo ya kisasa ya Tehama.
Awali Jaji Mkuu wa mahakama na Mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Asina Omary amesema kuwa zoezi la uboreshaji wa daftari la mpiga kura linatekelezwa mwa mujibu wa sheria kanuni na katiba ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya, aliwahimiza washiriki kuzingatia mafunzo hayo ili kufanikisha zoezi hilo kwa weledi na umakini mkubwa.
Mafunzo hayo yanafanyika kama maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Iringa, ambapo zoezi hilo litaanza rasmi tarehe 27 Desemba 2024 na kumalizika tarehe 02 Januari 2025.
MWISHO