Pambazuko FM Radio

IHI yatakiwa kuongeza elimu kwa wananchi

12 November 2026, 08:44

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa na viongozi na wadau wa IHI – picha na: Isidory Mtunda

Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete ameitaka Taasisi ya Afya ya Ifakara kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu shughuli na mafanikio yake, wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya taasisi hiyo.

Na: Isidory Mtunda

Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) imetakiwa kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli na mafanikio yake katika utafiti wa afya, ili jamii iweze kutambua mchango wa taasisi hiyo katika kukabiliana na changamoto za kiafya nchini na duniani.

Wito huo umetolewa na Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 70 ya IHI yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, kuelekea kilele chake kinachotarajiwa kufanyika siku ya Novemba 12, 2026.

Mh. Jakaya Kikwete – picha na: Isidory Mtunda

Amesema bado wananchi wengi hawafahamu kwa kina shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo licha ya mchango wake katika sekta ya afya.

Sauti ya rais mstaafu Jakaya Kikwete

Awali, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa IHI, Dkt. Ally Olotu, ametoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania, Serikali ya Uswisi na wadau wengine wa maendeleo kwa ushirikiano na uwekezaji wao katika utafiti wa afya. Amesema mafanikio ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka 70 yametokana na ushirikiano wa viongozi, watafiti na serikali mbalimbali zilizoamini katika matumizi ya sayansi na utafiti kutafuta suluhu za changamoto za kiafya

sauti ya mkurugenzi mtendaji wa IHI – DKT Ally Olotu

Maneno kwa lugha ya kiswahili:
Tungependa pia kuuenzi ushirikiano wa kudumu kati ya Serikali ya Tanzania na Uswisi, taasisi yetu mwanzilishi, pamoja na washirika wengine wengi ambao wamewekeza kwa watu wetu, katika miundombinu yetu, na kwenye malengo yetu ya kisayansi. Kwa washirika wetu wafadhili kama vile Serikali ya Uswisi, Wakfu wa Gates (Gates Foundation), EDCTP, Umoja wa Ulaya (European Union), Wellcome Trust — kuwataja wachache tu — pamoja na serikali za nchi nyingine rafiki kama vile Marekani, Uingereza, Ireland na nyinginezo; tungependa kusema asanteni kwa kutuamini na kuwekeza kwetu, na tunatarajia kuendelea kufanya kazi nanyi na kusukuma mbele ajenda yetu

Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini Tanzania ameipongeza IHI kwa mafanikio yake katika utafiti wa afya, akieleza kuwa nchi yake inajivunia kuwa miongoni mwa wadau wa mwanzo walioamini katika uwezo wa wanasayansi wa Afrika.

sauti ya Balozi wa Uswisi nchini Tanzania

Maneno kwa lugha ya kiswahili
Ni heshima na furaha kubwa kwangu kuungana nanyi leo kuadhimisha miaka 70 ya Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI). Miaka 70 ni hatua kubwa na ya kihistoria. Inawakilisha miongo saba ya uvumbuzi wa kisayansi, kujitolea kwa afya ya jamii, na azma ya pamoja ya kuboresha maisha ya watu nchini Tanzania na kwingineko. Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Uswisi, napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa IHI, uongozi wake, watafiti, wafanyakazi, na wote waliochangia katika safari hii ya kipekee. Leo, tunaadhimisha sio tu taasisi, bali pia ushirikiano. Ushirikiano ambao umekua kupitia kuaminiana, malengo ya pamoja, na imani thabiti kwamba sayansi na ushirikiano wa kimataifa vinaweza kuleta mabadiliko yenye maana katika maisha ya watu.

Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya Dkt Saitore Laizer amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutumia matokeo ya tafiti zake kuboresha sera za afya na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo pamoja na ustawi wa jamii.

Sauti ya Dkt Saitore Laizer kutoka wizara ya afya