Pambazuko FM Radio

Polisi wahimiza usalama wa matrekta

23 July 2026, 08:22

Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero limewataka wamiliki na madereva wa matrekta pamoja na power tiller kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kuhakikisha vyombo vyao vina taa, viakisi mwanga na madereva wanakuwa na leseni halali ili kupunguza ajali.

Na: Isidory Mtunda

Ajali nyingi zinazohusisha matrekta hutokea nyakati za usiku kutokana na baadhi ya matrekta kutokuwa na taa na viakisi mwanga (reflectors), hali inayosababisha kushindwa kuonekana na watumiaji wengine wa barabara.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kilombero, Mrakibu wa Polisi Blandina Kasongwa, wakati wa mkutano uliowakutanisha wamiliki wa matrekta, power tiller na madereva kutoka Tarafa ya Kidatu, uliofanyika katika Kituo cha Polisi Ifakara na kuhudhuriwa na zaidi ya wadau 50. Amesema kila dereva anapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuhakikisha chombo anachoendesha kinakidhi matakwa ya kisheria

DTO Kilombero Blandina Kasongwa
Sauti ya DTO Kasongwa

Naye Ofisa wa Polisi Jamii Wilaya ya Kilombero, SP Simpolianus Chacha, amewataka madereva kuhakikisha vyombo vyao vina taa na viakisi mwanga ili kuongeza usalama wa watumiaji wote wa barabara.

Sauti ya SP Chacha

Kwa niaba ya madereva, Mgalula Taifa Mgalula amesema baadhi ya madereva leseni zao zimekwisha muda na wengine hawana kabisa, hivyo ameliomba Jeshi la Polisi kuwapa muda wa kukamilisha taratibu za kupata leseni kwa kuwa shughuli hizo ndizo chanzo cha kipato cha familia zao.

Sauti ya Dereva – Mgalula

Akijibu ombi hilo, Mrakibu wa Polisi Blandina Kasongwa amesema atawasiliana na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro (RTO) ili wataalamu wafike wilayani humo kutoa mafunzo yatakayowawezesha madereva wengi kupata leseni kwa urahisi.

Sauti ya DTO

Kwa upande mwingine, Mkaguzi wa Magari Wilaya ya Kilombero, Sajenti Rajabu Juma Kadikarange, amewashauri wamiliki wa matrekta kuungana na kuwasilisha barua kwa DTO wa Wilaya ya Kilombero kuomba mafunzo hayo rasmi, akisema utaratibu huo utarahisisha madereva wengi kupata mafunzo na leseni kwa wakati mmoja.

Sauti ya mkaguzi Kadikarange