Pambazuko FM Radio

Polisi wafafanua mamlaka ya usalama barabarani

12 August 2026, 08:28

washiriki wa mafunzo kwa wamiliki na madereva wa vyombo vya moto kata ya Kiberege – picha na: WP9076 Mary Bayo

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kilombero, ASP Blandina Kasongwa, amefafanua mamlaka ya Polisi katika kudhibiti usalama barabarani, huku akiwataka madereva kutii maelekezo halali ya askari bila kujali aina ya sare anayovaa. Mazungumzo hayo pia yamejadili ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, taratibu za uhamisho wa umiliki wa vyombo vya moto na changamoto za bima.

Na: Isidory Mtunda

Baadhi ya madereva na watumiaji wa barabara wamekuwa wakihoji mamlaka ya askari wasiovaa sare za Traffic Police wanapowasimamisha au kuwapa maelekezo kuhusu usalama barabarani, huku baadhi yao wakikaidi maelekezo hayo kwa madai kuwa askari hao si askari wa usalama barabarani.

Akizungumza na wamiliki na madereva wa bodaboda, bajaji na maguta wa Kata ya Kiberege halmashauri ya mji wa Ifakara, mkuu wa kikosi cha usalama barabarani wilaya ya Kilombero, ASP Blandina Kasongwa, amesema suala la usalama barabarani ni jukumu la Jeshi la Polisi kwa ujumla, na si askari wa Traffic pekee.

ASP Blandina Kasongwa akitoa elimu ya usalama barabarani kwa wamiliki na madereva wa vyombo vya moto Kiberege – picha na: WP9076 Mary Bayo

Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 40 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na huduma saidizi, Jeshi la Polisi lina mamlaka ya kudhibiti na kusimamia traffic, hivyo kutokuwa na sare ya Traffic pekee hakumpi dereva msingi wa kupuuza maelekezo halali ya askari kuhusu usalama barabarani.

Sauti ya ASP Blandina Kasongwa

Kwa upande wao, mkuu wa kituo cha Polisi Kiberege, Staff Sergeant Thobias John, pamoja na Afisa elimu wa Kata ya Kiberege, Denice Kiwanuka, wamekemea tabia ya baadhi ya madereva wa bodaboda kubeba abiria zaidi ya mmoja, hususan wakati wa harusi na shughuli za michezo ya wanafunzi. Wameiomba DTO wa Kilombero kufuatilia changamoto hiyo na kuchukua hatua za kuhakikisha inakomeshwa.

Sauti ya OCS Thobias na Kiwanuka

Katika mkutano huo, washiriki pia walipata nafasi ya kuuliza maswali kwa mamlaka mbalimbali, ambapo baadhi ya maswali yalielekezwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yakihusu taratibu za kubadilisha umiliki wa vyombo vya moto pamoja na changamoto za upatikanaji na ukataji wa bima.

Sauti za washiriki wakiuliza maswali

Akijibu maswali hayo, Afisa wa TRA Ifakara, Bi. Witness Sonde, amesema mmiliki anayehitaji kubadilisha umiliki wa chombo cha moto anatakiwa kuwa na nyaraka za mauziano. Amesema endapo mmiliki wa awali amefariki, mwombaji anatakiwa kuwasilisha pia muhtasari wa kikao cha ndugu unaoonesha uhalali wa mchakato wa uhamisho wa umiliki

Sauti ya Witnes Sonde