Pambazuko FM Radio

Wafugaji 120 wapatiwa mafunzo ufugaji salama

1 May 2026, 20:09

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ufugaji wa kuku bora na salama – Picha kutoka maktaba – KV-HELP

Mafunzo hayo yanalenga kupunguza matumizi holela ya dawa za mifugo na kuboresha uzalishaji wa kuku katika Tarafa ya Kidatu.

Na; Isidory Mtunda

Zaidi ya wafugaji na wakulima 120 kutoka Tarafa ya Kidatu, Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro, wamepatiwa mafunzo ya ufugaji bora wa kuku ili kuboresha uzalishaji na kupunguza matumizi holela ya dawa za mifugo.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Taasisi ya KV-HELP kwa kushirikiana na Halmashauri ya mji wa Ifakara pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Francis (SFUCHAS), yakilenga kuwajengea wafugaji uelewa wa mbinu sahihi za ufugaji, kinga na tiba ya magonjwa ya kuku.

Akizungumza na Pambazuko FM, Afisa Mifugo wa Kata ya Msolwa Station ambaye pia alikuwa mwezeshaji wa mafunzo hayo, Emanuel Abraham, amesema kabla ya mafunzo walifanya tathmini iliyobaini changamoto kubwa za matumizi yasiyo sahihi ya dawa za mifugo pamoja na uwepo wa mabanda yasiyokidhi viwango.

Afisa mifugo kata ya Msolwa Station – Emmanuel Abraham – picha kutoka Maktaba
Sauti ya Afisa mifugo bwana Emmanuel Abraham

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Richard Andrew Mkine na Molecatherine Msowoya, wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha ufugaji wa kuku, ikiwemo utambuzi wa magonjwa na utoaji sahihi wa chanjo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ufugaji wa kuku bora na salama -picha na; Isidory Mtunda
sauti za wafugaji walioshiriki mafunzo – kidatu

Aidha, wafugaji hao wameeleza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya chanjo yamekuwa yakisababisha vifo vya kuku, na kupendekeza kuwepo kwa maabara maalum kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa ya kuku ili kuboresha huduma za tiba.

sauti ya mfugaji – Mohamed Mwisongo

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya KV-HELP, Iddy Mayumana, amesema mafunzo hayo yamepokelewa kwa mwitikio mkubwa, ambapo idadi ya washiriki imezidi matarajio katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kidatu, Mang’ula na Ifakara.

Mkurugenzi mtendaji wa KV-HELP- Mayumana – picha na; makta KV-HELP

sauti ya bwana Mayumana

Ameongeza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kubadilisha mtazamo na tabia za wafugaji kwa kuwahamasisha kutumia mbinu salama za ufugaji, ili kuongeza uzalishaji na kupunguza hasara zinazotokana na magonjwa ya mifugo.