Pambazuko FM Radio

Wananchi Kibaoni walalamikia ubovu wa barabara

13 May 2026, 20:18

Picha ya Barabara inayoelekea uwanja wa Ndege(Picha na Katalina Liombechi)

Wananchi wameiomba serikali kukarabati barabara hiyo haraka ili kuboresha mawasiliano na shughuli za kiuchumi.

Na Katalina Liombechi

Wananchi wa Kata ya Kibaoni katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara wameiomba serikali kutatua haraka ubovu wa barabara ya kuvuka reli kuelekea Uwanja wa Ndege, inayounganisha vitongoji vya Uwanja wa Ndege, Mji Mpya, Kilolelo, Kilama A na Kilama B.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uwanja wa Ndege, Jeremiah Machibya, amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa wa usafiri na usafirishaji wa mazao, hasa wakati huu mvua na kwamba magari kupita kwa shida, jambo linaloathiri biashara, wanafunzi na shughuli za kilimo.

Picha ya Mwenyekiti Kitongoji cha Uwanja wa ndege(Picha na Katalina Liombechi)
Mwenyekiti Kitongoji cha Uwanja wa ndege

Hata hivyo utakumbuka hivi Karibuni Mbunge wa Jimbo la Kilombero akiwa bungeni Jijini Dodoma alifikisha kilio hichio kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI akihoji nini mpango wa dharura wa serikali kutatua changamoto hiyo hasa wakati huu wa mavuno.

Kuhusiana na jambo hilo katika Majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI Dkt.Festo Dugange amesema serikali inatambua shughuli ya kilimo na uhitaji wa suluhu ya barabara katika eneo la Ifakara na kwamba tayari  kupitia kwa meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero na Mkoa wa Morogoro wameshafanya tathimini ya mahitaji ya matengenezo ya dharura,huku akiisisitiza TARURA Kufanya matengenezo maeneo waliyo na uwezo nayo ili kurahisisha wananchi  kupitisha mazao yao kwa wakati huu,wakati serikali ikiendelea na mkakati wa kuja na suluhu ya kudumu.

Picha ya Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mh. Abubakar Asenga(Picha kwa hisani ya Ofisi ya Mbunge Asenga)
Sauti ya Mh. Asenga na Naibu Waziri TAMISEMI