Pambazuko FM Radio

Madiwani Mlimba watakiwa kuhamasisha bima ya afya kwa wote

8 May 2026, 11:42

Picha ya Madiwani Halmashauri ya Mlimba katika kikao cha Baraza(Picha na Kuruthumu Mkata)

Bima ya afya kwa wote inapaswa kuwa ajenda kwenye mikutano ya maendeleo ya kata ili wananchi waweze kuelewa umuhimu wa kujiunga na mpango huo kujihakikishia huduma ya matibabu wanapougua

Na Kuruthumu Mkata

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, wakili Dumstan Kyobya, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Mlimba kuhakikisha wanahamasisha wananchi kujiunga na mpango wa bima ya afya kwa wote ili kuboresha huduma za afya katika jamii.

Akizungumza katika Mkutano wa Kawaida wa baraza la madiwani wa robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2025/2026, uliofanyika katika Mlimba, Mkuu huyo wa Wilaya amesema madiwani wanapaswa kulisimamia kwa karibu suala la bima ya afya na kulijadili katika mikutano ya maendeleo ya kata zao ili wananchi waweze kuelewa umuhimu wa kujiunga na mpango huo.

Ameeleza kuwa Serikali tayari imetoa huduma ya bima ya afya kwa gharama ya shilingi laki moja na nusu, ambapo watu sita wa familia moja wanaweza kupata matibabu katika hospitali zote nchini.

Kutokana na fursa hiyo, aliwataka madiwani kutumia nafasi zao kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na mpango huo muhimu.

Picha ya Mh. Dunstan Kyobya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero

Katika hatua nyingine, Wakili Dunstan Kyobya amezungumzia suala la matumizi ya vyandarua vilivyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na malaria huku akisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakivitumia kwa matumizi yasiyo sahihi huku wengine wakiviuza badala ya kuvitumia kwa lengo lililokusudiwa.

Hata hivyo Kutokana na hali hiyo, ameagiza wananchi ambao hawakupata vyandarua kuandikishwa ili waweze kupatiwa vingine kupitia utaratibu wa Serikali, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia vyandarua hivyo kwa ajili ya kujikinga dhidi ya malaria.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amegusia suala la mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri kwa vikundi mbalimbali vya wananchi ambapo amesema mikopo hiyo inapaswa kutolewa katika kata zote kwa usawa, huku akielekeza kuwa katika Halmashauri ya Mlimba kuna kata mbili ambazo utaratibu wake unapaswa kurekebishwa na kurudiwa upya ili kuhakikisha haki inatendeka.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya Vyandarua

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlimba, Bi Martha Mkula, amesema maendeleo ya halmashauri hiyo yanategemea mahusiano mazuri, ushirikishwaji na mshikamano miongoni mwa viongozi na wananchi na kusisitiza kuwa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo utaifanya Halmashauri ya Mlimba kusonga mbele zaidi.

Picha ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlimba Martha Mkula(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlimba Martha Mkula