Pambazuko FM Radio

DC Kyobya awataka wafugaji kufuga kisasa

17 August 2026, 21:33

DC akikagua malisho kwaajili mifugo – picha na: Kuruthum Mkata

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amewasihi wafugaji kuiga mfano wa Mfugaji Bora wa Mkoa wa Morogoro, John Kasekele, kwa kufuga kisasa na kwa tija ili kukuza uchumi na kuepusha migogoro na wakulima. Hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dk. Dunia Mlanzi, ilisisitiza umuhimu wa kufuata vigezo vya kitaalamu vya ufugaji ili mkoa huo uweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kitaifa yajayo.

Na: Kuruthum MKata

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amewataka wafugaji kuachana na ufugaji wa kizamani na kukumbatia mbinu za kisasa na zenye tija ili kuongeza uzalishaji na kupunguza migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.

Ameyasema hayo leo, Agosti 17, 2026, katika hafla ya kumpongeza Mfugaji Bora wa Mkoa wa Morogoro kupitia Maonesho ya Nanenane 2026, iliyofanyika nyumbani kwa mshindi huyo. Katika hafla hiyo, DC Kyobya amezitaka halmashauri kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wafugaji kufuga kitalamu na kuwataka wafugaji wengine kuiga mfano wake.

DC wakili Kyobya akielekeza jambo – picha na: Kuruthum Mkata
Sauti ya DC Kyobya akitoa neno wakati wa hafla hiyo

Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dk. Dunia Mlanzi, amempongeza mshindi huyo na kueleza kuwa uteuzi ulizingatia vigezo vya kitaalamu. Amewahimiza wakulima na wafugaji kufuata nyayo hizo ili kuiwezesha Mkoa wa Morogoro kufanya vizuri zaidi na kushinda katika ngazi ya kitaifa mwakani.

Dkt Dunia Mlanzi akitoa neno la pongezi kwa bwana John Kasekele – picha na: Kuruthum Mkata
Sauti ya Dkt Dunia Mlanzi

Naye Mfugaji Bora wa Mkoa wa Morogoro, John Chambi Kasekele, amewashauri wafugaji wenzake kujikita katika ufugaji wa mkibiashara, kusomesha watoto wao, na kuhakikisha shughuli hiyo inaleta tija halisi. Amesema hatua hiyo itasaidia kuinua maisha yao kiuchumi na kuondoa migogoro ya ardhi na wakulima.

Bwana John Chambi Kasekele, mfugaji bora mkoa wa Morogoro nane nane 2026 – picha na: Kuruthum Mkata
Sauti ya bwana John Kasekele