Pambazuko FM Radio

AWF yatambuliwa kuinua kilimo cha kakao Mlimba

16 May 2026, 09:59

Picha ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mh.Dunstan Kyobya akimkabidhi cheti Alexander Mpwaga kwa niaba ya AWF(Picha na Kuruthumu Mkata)

AWF inajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kuhamasisha wananchi kujikita kwenye kilimo cha kakao ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa SUSTAIN-ECO

Na Katalina Liombechi/Kuruthumu Mkata

Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Afrika (AWF) umetunukiwa cheti cha kutambuliwa kama mmoja wa wadau waliofanikiwa kuhamasisha na kukuza zao la kakao katika Halmashauri ya Mlimba kutokana na mchango wake mkubwa katika kuwawezesha wakulima pamoja na kukuza kilimo hicho chenye tija kwa jamii.

Cheti hicho kilichotolewa na Mkurugenzi wa Halmashuari ya Mlimba kilikabidhiwa Mei 14, 2026 katika uzinduzi wa Siku ya Mkulima wa Kakao uliofanyika katika Kata ya Mbingu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa kilimo, viongozi wa serikali pamoja na wakulima wa zao la kakao ambapo taasisi zaidi ya 18 kutoka maeneo tofauti ya bonde la Kilombero zilishiriki maonesho hayo na kuwezesha wakulima kupata Teknolojia,maarifa na na fursa za kuboresha kilimo na biashara ya kakao.

Akizungumza mara baada ya kupokea cheti hicho kwa niaba ya AWF, Mchumi Kilimo wa Mfuko huo, Alexander Mpwaga, amesema kuwa AWF inajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kuhamasisha wananchi kujikita kwenye kilimo cha kakao akieleza kuwa tangu mwaka 2017, AWF imechangia ongezeko la wakulima wa kakao kutoka 2,169 hadi 5,968, huku uzalishaji ukiongezeka kutoka tani 347 hadi zaidi ya tani 1,001 na kwamba wakulima wamejiingizia zaidi ya Shilingi bilioni 5  katika msimu uliopita.

Kwa mujibu wa Mpwaga, mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa Mradi wa Sustain Eco , ambao ulifadhiliwa na Serikali ya Sweden.

Mradi huo wa miaka mitatu ulikuwa na lengo la kurejesha mifumo ikolojia katika Bonde la Kilombero ambapo katika zao la kakao ulikusudia kuwainua wananchi kiuchumi kupitia shughuli endelevu za uzalishaji.

Kupitia mradi huo, AWF wakishirikiana na Shirika linalojihusisha na uhifadhi wa mazingira Duniani IUCN walijikita katika kutoa mafunzo kwa Maafisa ugani na wakulima wa kakao, kuwapatia teknolojia pamoja na kuwajengea uwezo wa kuzalisha miche bora ya kakao ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo.

Picha ya Alexander Mpwaga Mchumi Kilimo AWF(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Mpwaga AWF

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero wakili Dunstan Kyobya, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo uzinduzi wa siku ya mkulima wa Kakao, akikabidhi cheti hicho alisema AWF imekuwa mfano mzuri wa taasisi zinazounga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha kilimo cha kakao, ambacho ni miongoni mwa mazao ya kimkakati katika Mkoa wa Morogoro.

Aidha, amewataka wakulima wa kakao kuendelea kuwa mabalozi wa zao hilo kwa kuwahamasisha wananchi wengine kujiunga na kilimo hicho ili waweze kujikwamua kiuchumi na kupunguza utegemezi wa matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za asili kujipatia kipato.

Kupitia Uzinduzi wa Siku ya Mkulima wa Kakao ikiwa ni wazo lililobuniwa na kuzinduliwa kwa ufadhili wa AWF, Mkuu wa wilaya ameagiza siku hiyo iwe inaadhimisha kila mwaka ikitajwa kuwa chachu mpya ya kuimarisha kilimo cha kakao katika Bonde la Kilombero.

Picha ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Mkuu wa Wilaya

Wadau mbalimbali wamesesitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika zao hilo kwa manufaa ya uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla huku Mkuu wa Idara ya Kilimo katika Halmashauri hiyo Romanus Myeye amesema wataendelea kuwasimamia wakulima na kuendelea kuwahamasisha wengine zaidi ili kuendelea kuenzi mchango wa AWF kwa kulipa thamani zao la Kakao.

Tutaendelea kuwasimamia na kuhamasisha zaidi wakulima kulima zao la kakao kwa sababu sisi kama halmashauri linatuweka juu kimapato na limewasaidia wananichi kuinuka kiuchumi

Picha ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero akikagua banda la kokoa(Picha na Kuruthumu Mkata)