Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
24 July 2026, 09:10

Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero limetoa elimu ya usalama barabarani kwa wamiliki na madereva wa matrekta na power tiller wa Tarafa ya Mang’ula, likiwataka kuzingatia sheria ili kupunguza ajali.
Na: Isidory Mtunda
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero limesema wamiliki na madereva wa matrekta pamoja na power tiller katika Tarafa ya Mang’ula wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za usalama barabarani, zikiwemo ukosefu wa leseni halali, kutosajili vyombo vyao, ukosefu wa mfumo wa umeme na honi, pamoja na kuendesha vyombo hivyo bila kukaguliwa.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya usalama barabarani yaliyowahusisha zaidi ya wamiliki na madereva 100 wa matrekta na power tiller, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mang’ula, ASP Montanus Mchopa, amesema changamoto hizo zinahatarisha usalama wa madereva na watumiaji wengine wa barabara na amewataka kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Baada ya mafunzo hayo, washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali, ambapo mmoja wa washiriki, Kapesa Msangi, alieleza changamoto wanazokumbana nazo wanapofika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufuatilia usajili wa matrekta, akisema baadhi ya matrekta hukosa namba za utambuzi (chassis number), jambo linalochelewesha usajili.
Akijibu hoja hiyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kilombero, Mrakibu wa Polisi Blandina Kasongwa, amesema ili trekta lisajiliwe, mmiliki anatakiwa kukamilisha matakwa yote ya kisheria, ikiwemo kufunga mfumo wa umeme na kulipeleka likaguliwe na mkaguzi wa magari kabla ya kusajiliwa.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Magari na Mtahini wa Madereva Wilaya ya Kilombero, Sajenti Rajabu Juma Kadikarange, amewataka madereva kuacha tabia ya kubeba watu juu ya mizigo kwenye matrekta na power tiller, akisema ni ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani unaoweza kusababisha ajali na kuhatarisha maisha ya wananchi.
