Pambazuko FM Radio

KV-HELP yawainua wafugaji wa Kuku

30 June 2026, 11:52

Wafugaji wa kuku katika Kata ya Mwaya wamepatiwa mafunzo ya utambuzi wa magonjwa, kinga na mbinu bora za ufugaji ili kuongeza uzalishaji na kupunguza hasara.

Na: Henry Mwakifuna

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ufugaji wa kuku yaliyofanyika katika Kata ya Mwaya, Tarafa ya Mangula, Halmashauri ya Mji Ifakara, wamesema ukosefu wa elimu ya kutambua magonjwa ya kuku umekuwa kikwazo kikubwa katika shughuli zao za ufugaji.

Washiriki hao wamesema changamoto hiyo imesababisha baadhi ya wafugaji kuacha kabisa shughuli za ufugaji wa kuku, huku wengine wakipoteza mitaji kutokana na vifo vya mifugo yao kwa kushindwa kutambua dalili za magonjwa na kuchukua hatua kwa wakati.

sauti za washiriki wa mafunzo

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kilombero Valley Healthy and Livelihood Promotion (KV-HELP), Daktari Salieri Eliabu kutoka kampuni ya Silverlands Tanzania Limited amesema kinga ndiyo msingi wa mafanikio katika ufugaji wa kuku.

Dkt. Eliabu wa Silverland Iringa

Amesema wafugaji wanapaswa kuhakikisha wanazingatia usafi wa mazingira ya kufugia, kuimarisha ulinzi wa shamba dhidi ya maambukizi ya magonjwa (biosecurity), pamoja na kuwapatia kuku chanjo kwa wakati kabla ya magonjwa kujitokeza.

Sauti ya Dkt Eliabu

Naye Diwani wa Kata ya Mwaya, Anthony Mwampunga, amesema mafunzo hayo yatawawezesha wafugaji kuboresha mbinu zao za ufugaji, kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha kaya. Amehimiza Halmashauri ya Mji Ifakara kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kutoa mafunzo yanayowajengea uwezo wafugaji.

Sauti ya Diwani Mwampunga

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kilombero Valley Healthy and Livelihood Promotion (KV-HELP), Iddy Mayumana, amesema lengo la mradi wa Kuku Salama ni kuwawezesha wafugaji kufuga kuku kwa kuzingatia kanuni bora za ufugaji, kupunguza matumizi yasiyo sahihi ya dawa za mifugo, na kufuata ushauri wa wataalamu ili kuongeza uzalishaji wa kuku wenye afya.

Bwana Iddy Mayumana mkurugenzi KV-HELP
Sauti ya mkurugenzi wa KV-HELP – I. Mayumana

Mafunzo hayo yameandaliwa na KV-HELP kwa kushirikiana na Wataalamu wa Mifugo kutoka Halmashauri ya Mji Ifakara pamoja na kampuni ya Silverlands Tanzania Limited ya mkoani Iringa, yakilenga kuwajengea uwezo wafugaji katika utambuzi wa magonjwa, kinga, na mbinu bora za ufugaji wa kuku.