Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
14 May 2026, 11:28

Maafisa wa mazingira na mifugo wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara wamewataka wananchi wanaofuga mifugo mijini kufuata sheria na taratibu za ufugaji salama ili kulinda mazingira, afya za wananchi na kuepusha migogoro kati ya wafugaji na jamii.
Na: Isidory Mtunda
Maafisa wa mazingira na mifugo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro wamewataka wananchi wanaojihusisha na ufugaji mijini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ufugaji salama ili kuepusha athari kwa mazingira na jamii.
Akizungumza na Pambazuko FM Radio, Afisa Mazingira wa Halmashauri hiyo, Salome Mayenga amesema ni kosa kisheria kuzungusha mifugo katika maeneo ya mjini kwa lengo la kutafuta malisho, akieleza kuwa wafugaji wanapaswa kuandaa malisho au kukata majani na kuyapeleka moja kwa moja zizini.
Insert: Mayenga – CLIP
Naye Afisa Mifugo wa Kata ya Msolwa Station, Emanuel Abraham amesema shughuli za ufugaji mjini zinaruhusiwa kisheria, lakini wafugaji wanatakiwa kufuga idadi ya mifugo wanayoweza kuihudumia ndani ya mabanda au mazizi bila kuathiri mazingira na wananchi wengine.

Kwa upande wao, baadhi ya wafugaji wa Kata ya Mlabani wameeleza changamoto wanazokutana nazo katika shughuli za ufugaji mijini. Mfugaji wa nguruwe, Castor Joseph Mlango amesema hulazimika kufuga nguruwe wake ndani ya banda, ingawa wakati mwingine hutoka na kuingia kwenye mashamba ya wananchi kutokana na upungufu wa chakula. Naye mfugaji wa ng’ombe, Upendo Gabrieli Munsa amesema baadhi ya ng’ombe hukataa kula majani yaliyokatwa, hali inayowalazimu kuwapeleka katika maeneo ya wazi kwa ajili ya malisho.