Pambazuko FM Radio

Viongozi wa mila watakiwa kulinda maadili

14 May 2026, 10:37

Afisa utamaduni wa halmashauri ya mji wa Ifakara amewataka viongozi wa kimila kuendelea kusimamia maadili ya jamii kwa kukemea vitendo vinavyokiuka mila na desturi za Kitanzania, ikiwemo ushoga na ndoa za jinsia moja.

Na: Isidory Mtunda

Viongozi wa kimila wametajwa kuwa na mchango muhimu katika kuhifadhi mila, desturi na maadili ya jamii, sambamba na kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali katika ngazi ya kijamii.

Majaliwa Mbughi – afisa utamaduni mji wa Ifakara

Akizungumza na Pambazuko FM Radio, Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro, Majaliwa Mbugi amesema serikali inaendelea kutambua nafasi ya viongozi wa kimila katika jamii, hususan katika kusimamia maadili na kukemea vitendo vinavyokiuka mila na desturi za Kitanzania, ikiwemo ndoa za jinsi moja na ushoga.

Sauti ya afisa utamaduni – Majaliwa Mbughi

Naye Chief Solyambingu II Towegale Kiwanga wa kijiji cha Utengule, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba amesema viongozi wa kimila bado wana nafasi kubwa katika jamii, lakini wakati mwingine ushiriki wao katika shughuli za maamuzi ya kijiji huwa mdogo kutokana na kutohusishwa mara kwa mara katika mikutano ya serikali za vijiji.

Ameongeza kuwa baadhi ya kauli zao hazipewi uzito wa kutosha licha ya uzoefu wao katika masuala ya mila, utatuzi wa migogoro na malezi ya maadili katika jamii.

Sauti ya chief Solyambingu

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Utengule, Hassan Omary Pamuhi amesema viongozi wa kimila wanaendelea kuwa sehemu muhimu ya jamii kwa kusimamia shughuli za kimila na kusaidia kuhamasisha mshikamano wa wananchi.

Amepongeza ushiriki wa Chief Solyambingu II Towegale Kiwanga katika shughuli mbalimbali za kijiji na kueleza kuwa ushirikiano kati ya serikali ya kijiji na viongozi wa kimila una umuhimu mkubwa katika maendeleo ya jamii.

Sauti ya mtendaji wa kijiji – Hassan Pamuhi