Pambazuko FM Radio

Hakirasilimali yatoa elimu ya madini

29 June 2026, 13:19

washiriki wa semina ya haki za madini Mahenge Ulanga – picha na; Isidory Mtunda

Wananchi wa vijiji vya Epanko, Kisewe na Mdindo wilayani Ulanga wamepata elimu kuhusu haki za madini, fidia na ushiriki wao katika miradi ya uwekezaji, huku wakipata fursa ya kuhoji masuala mbalimbali yanayohusu mgawanyo wa mapato na manufaa ya rasilimali za madini

Na: Isidory Mtunda

Wananchi wa vijiji vya Epanko, Kisewe na Mdindo wilayani Ulanga wameitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu mgawanyo wa mapato ya madini na masuala ya fidia, wakieleza wasiwasi wao juu ya kile wanachokiona kuwa ni kipaumbele kikubwa kwa wawekezaji kuliko wananchi wanaoathiriwa na shughuli za uchimbaji madini. Akizungumza wakati wa semina ya uelewa wa haki za rasilimali iliyoandaliwa na shirika la Hakirasilimali, Paroko wa Parokia ya Epanko, Padre Manifred Rufino Mkopa, amehoji kuhusu asilimia 16 ya hisa ambazo serikali hupata katika miradi ya madini na kuhoji iwapo maslahi ya wananchi yanazingatiwa ipasavyo katika uwekezaji huo.

Sauti ya Padre Manifred

Akijibu hoja hiyo, Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Zawadi Mtatifikolo, amesema mgawanyo wa asilimia 16 kwa serikali na asilimia 84 kwa mwekezaji huanza kutumika baada ya uzalishaji wa madini kuanza na si kabla ya mradi kuanza kufanya kazi.

sauti ya afisa ardhi Mtatifikolo

Kwa upande wake, Afisa Programu kutoka Hakirasilimali, Francis Mkasiwa, amefafanua kuwa umiliki wa asilimia 16 wa serikali ulitokana na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017, ambapo serikali huingia ubia katika miradi ya madini kupitia hisa zisizolipiwa.

Sauti ya Francis Mkasiwa

Aidha, Mtatifikolo amekanusha madai kuwa serikali imekuwa ikiwapa upendeleo wawekezaji kuliko wananchi, akieleza kuwa kabla ya utekelezaji wa miradi mbalimbali hufanyika vikao vya ushirikishwaji wa wananchi pamoja na makubaliano ya viwango vya fidia kwa maeneo yanayoathiriwa.

Sauti ya afisa ardhi Mtatifikolo

Naye Francis Mkasiwa amesema semina hiyo imewakutanisha washiriki 51 wakiwemo viongozi wa vijiji, halmashauri, taasisi za dini na asasi za kiraia kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na ushiriki wao katika maamuzi yanayohusu rasilimali za madini.

Sauti ya Francis Mkasiwa