Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
23 June 2026, 19:13

Mazingira rafiki na wezeshi yanaongeza fursa za ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa eneo la Ifakara na Wilaya ya Kilombero kwa ujumla.
Na Katalina Liombechi
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji, hususan wazawa, jambo ambalo limekuwa likirahisisha na kuvutia uwekezaji wenye manufaa kwa taifa na wananchi.
Akizungumza Juni 22, 2026, wakati alipotembelea ya kisasa ya COC Hotel iliyopo Kata ya Mbasa, Ifakara, na ambayo imeanza kutoa huduma hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya huyo amesema uwekezaji huo unaongeza mvuto wa Mji wa Ifakara kwa wageni na wadau wanaofika eneo hilo kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Ziara hiyo imehusisha pia wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, ambapo walipata fursa ya kujionea huduma na miundombinu iliyowekwa katika hoteli hiyo na kushauri mambo mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Chipa Omary Chikwekwe, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini, hali ambayo imekuwa chachu ya ukuaji wa uwekezaji.
Pia ameeleza kuridhishwa kwake na ushirikiano anaoupata kutoka kwa Halmashauri ya Mji wa Ifakara pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero.
Amesema mazingira bora ya biashara na uwekezaji yaliyopo yamechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha ujenzi na uendeshaji wa hoteli hiyo, ambayo inatarajiwa kuongeza fursa za ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa eneo la Ifakara na Wilaya ya Kilombero kwa ujumla.
