Pambazuko FM Radio

Jamii Kibaoni yalaani vitendo vya ukatili wa kijinsia

14 May 2026, 19:15

Picha ya Polisi Kata Kibaoni akitoa elimu ya Ukatili wa Kijinsia(Picha na Katalina Liombechi)

Matukio ya ukatili wa kijinsia sio mara ya kwanza kutokea katika kitongoji cha milola

Na katalina Liombechi

Wananchi wa kitongoji cha Milola, Kijiji cha Kibaoni Halmashauri ya mji wa Ifakara wameeleza kutoridhishwa na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yanayoendelea kutokea katika eneo hilo, huku wakiyalaani vikali matukio ya namna hiyo.

Hatua hiyo inafuatia tukio la mwanamke mmoja ambaye majina yake kamili bado hayajafahamika, kudaiwa kushambuliwa kwa kutumia vitu vyenye ncha kali na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

Tukio hilo linadaiwa kutekelezwa na mume wake anayefahamika kwa jina la Juma Liwawa, usiku wa Mei 10, 2026.

Picha ya baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Milola-Kibaoni(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za wananchi Milola Kibaoni

Akizungumza mara baada ya kutoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia Mei 13,2026 katika Kitongoji hicho akizungumzia tukio hilo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kata ya Kibaoni, Makamba, amesema kuwa mwanamke huyo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisko iliyopo Ifakara, huku mtuhumiwa akiendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Aidha, kupitia tukio hilo, Mkaguzi Msaidizi huyo wa Polisi ameitaka jamii kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa wanaposhuhudia au kuona viashiria vya vitendo vya ukatili, ili kusaidia kukomesha matukio hayo mapema katika jamii kwani amesema matukio ya namna hiyo sio mara ya kwanza kutokea katika eneo hilo na kwamba wanaendelea kutoa elimu kuibadilisha jamii.

Picha ya Polisi Kata ya Kibaoni akitoa Elimu ya Ukatili wa Kijinsia(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Polisi kata Kibaoni