Walimu wanufaika na mafunzo ikolojia,ufugaji nyuki
Walimu wanufaika na mafunzo ikolojia,ufugaji nyuki
18 June 2026, 20:36
Picha ya Mgeni rasmi,Viongozi Six rivers Africa na wanufaika wa mafunzo(Picha na Katalina Liombechi)
Shirika la Six rivers Africa limetoa mafunzo hayo likiamini kuwa elimu ya ikolojia inayowafikia wanafunzi kupitia walimu wao itachangia kujenga kizazi chenye uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira
Na Katalina Liombechi
Shirika la Six Rivers Africa limetoa mafunzo ya siku tatu kwa walimu kutoka shule 16 za msingi zinazopakana na Hifadhi ya Nyerere yakilenga kuimarisha uendeshaji wa klabu za ikolojia mashuleni pamoja na kuwajengea uwezo katika shughuli za ufugaji nyuki.
Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha walimu kuwa mabalozi wa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wanafunzi wao, huku yakihamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za asili na fursa za kiuchumi zinazotokana na uhifadhi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Meneja wa Matokeo wa Six Rivers Africa, Mary Marandu, amesema shirika hilo linaamini kuwa elimu ya ikolojia inayowafikia wanafunzi kupitia walimu wao itachangia kujenga kizazi chenye uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Picha ya Mary Marandu Meneja wa Matokeo wa Six Rivers Africa(Picha na Katalina Liombechi)
Tunaamini kupitia mafunzo haya, vijana wadogo watapata fursa ya kuelewa na kuiishi dhana ya uhifadhi wa mazingira. Watatambua kuwa maisha ya binadamu na viumbe wengine yanategemeana na kwamba ushirikiano huo unapaswa kuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho
Aidha, amesema mafunzo hayo yanatoa nafasi kwa walimu kujifunza mbinu bora za ufugaji nyuki, shughuli ambayo imeonekana kuwa chanzo muhimu cha kipato kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi huku ikichangia uhifadhi wa mazingira kupitia uchavushaji wa mimea na ulinzi wa misitu.
Mgeni rasmi aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, katika mafunzo hayo Rashid Semgoya, amewataka walimu pamoja na wanajamii kutumia maarifa watakayoyapata kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi na kueneza elimu hiyo kwa wengine.
Picha ya Rashid Semgoya Mwakilishi Semgoya(Picha na Katalina Liombechi)Sauti ya Mgeni rasmi Semgoya
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo walikuwa na haya ya kusema
Picha ya Washiriki wakipatiwa mafunzo(Picha na Katalina Liombechi)Sauti za walimu wanufaika mafunzo ya Ikolojia na ufugaji nyuki
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia June 15,2026 katika ukumbi wa Edger Marantha yanatarajiwa kuimarisha ushiriki wa shule za msingi na jamii katika shughuli za uhifadhi wa mazingira, huku yakikuza uelewa wa umuhimu wa kulinda bioanuwai na kutumia rasilimali za asili kwa njia endelevu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.