Pambazuko FM Radio

Mlimba kuwapeleka wataalamu Zanzibar

11 August 2026, 08:52

Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea banda la Mlimba kwenye nane nane

Halmashauri ya Mlimba imepanga kupeleka wataalamu wake Zanzibar kwa mafunzo ya kilimo cha mazao ya viungo, kufuatia ushauri wa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete. Hatua hiyo inalenga kuongeza ujuzi wa wataalamu na kuboresha uzalishaji wa mazao ya viungo, huku halmashauri ikitangaza pia mpango wa kugawa miche ya kakao bure kwa wakulima.

Na: Henry Mwakifuna

Halmashauri ya Mlimba imepanga kupeleka wataalamu wake Zanzibar kwa mafunzo maalumu ya kilimo cha mazao ya viungo, hatua inayolenga kuongeza ujuzi na kuimarisha uzalishaji wa mazao hayo kwa wakulima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Jamary Idrisa Abdul, ameiambia Pambazuko FM kuwa uamuzi huo umechochewa na ushauri uliotolewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, baada ya kutembelea banda la Mlimba katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Jamary, Dkt. Kikwete alishauri wataalamu wa halmashauri hiyo kwenda Zanzibar kujifunza zaidi kuhusu kilimo cha mazao ya viungo baada ya kuelezwa na Afisa Kilimo wa Mlimba, Romanus Myeye, kuwa tayari wamepata mafunzo ya awali kutoka Morogoro Vijijini.

Katika hatua nyingine, Jamary ametangaza kuwa kuanzia msimu huu wa kilimo cha kakao, Halmashauri ya Mlimba itagawa miche bure kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kukuza mchango wa zao hilo katika uchumi wa wananchi.

Aidha, amesema halmashauri hiyo itaendelea kuwekeza katika ubunifu na teknolojia za kilimo ili kudumisha mafanikio yake baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kati ya halmashauri tisa za Mkoa wa Morogoro kwenye Maonesho ya Nanenane mwaka huu.

Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Mlimba – Jamary Idrisa Abdul akiwa kwenye maeneo ya Vipando – picha na; Isidory Mtunda
Sauti ya Jamary Idrisa Abdul