Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
8 September 2026, 12:51

Morogoro yaripoti matukio 2,129 ya uhalifu wa mtandao, huku Kilombero ikiongoza kwa matukio 1,780.
Na: Kuruthum Mkata
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema Mkoa wa Morogoro umeripoti matukio 2,129 ya uhalifu wa mtandao, huku Wilaya ya Kilombero ikiongoza kwa kuripoti matukio 1,780.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa mawasiliano, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema Ifakara ni miongoni mwa maeneo yanayoathirika zaidi na uhalifu huo, huku TCRA ikiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na uhalifu wa mtandao.

mkurugenzi mkuu TCRA mhandisi Peter Mwasalyanda – picha na: Kuruthum Mkata
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amekiri kuwepo kwa changamoto ya wizi wa kimtandao katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, akitaja Kata za Lumemo na Lipangalala kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa matukio hayo.
Amesema wananchi wanapaswa kulinda laini zao za simu na kuhakikisha hazitumiki na watu wengine, huku akiwataka kutoa taarifa kuhusu matukio ya uhalifu wa mtandao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Kwa upande wao, baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, akiwemo Diwani wa Kata ya Ifakara, Khalfan Mteke, wamekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuwataka wananchi kuwa makini wanapotumia huduma za mtandaoni.