Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
23 September 2026, 18:07
Wengi hususan mabinti, hukumbana na vishawishi mbalimbali kutoka kwa marafiki, mazingira na hata hali ngumu za kifamilia, jambo linalowafanya baadhi yao kukata tamaa na kuacha kuzingatia masomo-Innosencia Ngadaya

Na Henry Mwakifuna
Wanafunzi wametakiwa kutokata tamaa wanapokutana na changamoto za maisha na badala yake kuzitumia kama chachu ya kufikia ndoto zao za kielimu na maendeleo ya baadaye.
Akizungumza kuhusu changamoto za masomo, kupitia Tuzungumze Elimu ya Pambazuko FM Innosensia Ngadaya amesema wanafunzi wengi, hususan mabinti, hukumbana na vishawishi mbalimbali kutoka kwa marafiki, mazingira na hata hali ngumu za kifamilia, jambo linalowafanya baadhi yao kukata tamaa na kuacha kuzingatia masomo.

Ngadaya amesisitiza umuhimu wa kuchagua marafiki wenye ushawishi chanya, kujisimamia binafsi na kuepuka kujilinganisha na wengine. Amesema maisha magumu ya sasa hayamaanishi mtu ataendelea kuwa katika hali hiyo milele iwapo ataendelea kujituma na kusoma kwa bidii.
sauti ya Innocensia Ngadaya
Kwa upande wake, Mwalimu aliyemsimamia kwa Muda mrefu katika Taaluma yake, Martinny Mianjam amesema changamoto zinapaswa kutazamwa kama fursa ya kujifunza na kujenga uimara wa kukabiliana na maisha. Amesema watu wengi waliofanikiwa walipitia changamoto mbalimbali lakini hawakukata tamaa.
Aidha, amewahimiza wanafunzi kutafuta ushauri na msaada wanapokumbana na matatizo, akibainisha kuwa wanaokabiliana na changamoto zao kwa ujasiri na kuzitafutia suluhisho mara nyingi ufikia mafanikio makubwa.
sauti ya Mwalimu Martiny Mianjam