Pambazuko FM Radio

Wafanyabiashara Ifakara Wahimizwa kujitokeza kliniki ya kodi

29 October 2026, 15:31

Maafisa wa TRA Innocent Minja wa Kilombero ( Kushoto ) na Chacha Gotola wa Mkoa wa Morogorp (Kati ) wakitoa Elimu katika Studio za Pambazuko FM picha na Joel Huruki

Kupitia kliniki hiyo, wafanyabiashara wanapata elimu kuhusu wajibu wa kujisajili kwa hiari, utunzaji sahihi wa kumbukumbu za biashara, uwasilishaji wa marejesho ya kodi (returns) na masuala mengine yanayohusu ulipaji wa kodi.-Chacha Gotola

Na Henry Mwakifuna

Wafanyabiashara wa Mji wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, wamehimizwa kuendelea kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Kodi inayotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa lengo la kupata ufumbuzi wa changamoto zinazohusiana na masuala ya kodi na uendeshaji wa biashara zao.

Akizungumza na Pambazuko FM, Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Walipa Kodi Mkoa wa Morogoro, Chacha Gotola, amesema kliniki hiyo imewakutanisha wataalamu kutoka Makao Makuu ya TRA, mkoa na wilaya, hatua inayowapa wafanyabiashara fursa ya kupata huduma na ufafanuzi wa changamoto zao kwa urahisi.

sauti ya Chacha Gotola

Meneja wa TRA Wilaya ya Kilombero, Innocent Minja, akitoa ufafanuzi juu ya Kliniki ya Kodi Ifakara Picha na Joel Huruki

Akizungumzia umuhimu wa wafanyabiashara kutangaza biashara zao kupitia mitandao ya kijamii na vituo vya redio, Meneja wa TRA Wilaya ya Kilombero, Innocent Minja, amesema matangazo ni sehemu muhimu ya kukuza biashara na kwamba kila mfanyabiashara ana haki ya kutangaza bidhaa na huduma zake.

Minja amesema biashara ni chanzo muhimu cha kukuza uchumi na kutengeneza ajira, huku akiwahimiza wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi na kusisitiza kuwa TRA inalenga kuhakikisha biashara zinaendelea kwa kuzingatia sheria za kodi.

sauti ya Innocent Mjinja

Kliniki ya Kodi Ifakara imefanyika kufuatia maelekezo ya Kamishna Mkuu wa TRA baada ya kukutana na wawakilishi wa wafanyabiashara wa Wilaya ya Kilombero Oktoba 19, mwaka huu.

Wafanyabiashara wametakiwa kutumia fursa hiyo kupata ufafanuzi wa changamoto zao na kuzingatia elimu inayotolewa ili kuimarisha utii wa sheria za kodi na kukuza biashara zao.