Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
10 November 2026, 11:31

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira wakikagua Mto Lumemo Ifakara Picha na Kuruthum Mkata
Wananchi Shirikianeni na Serikali katika Kutunza Vyanzo vya Maji na msifanye Shughuli za Kilimo kandokando ya Mito–Kamati ya Bunge
Na Kuruthum Mkata
Wananchi wa Wilayani Kilombero mkoani Morogoro wametakiwa kushirikiana na Serikali katika kulinda vyanzo vya maji, ikiwemo Mto Lumemo, ili kuzuia athari za mafuriko yanayojitokeza katika maeneo ya Ifakara.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Mhe. Jackson Kiswagwa (MB), wakati wa ziara ya kamati hiyo kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko katika Mto Lumemo, Ifakara,ambapo amewataka wananchi kuacha shughuli za kilimo kandokando ya mto na kushiriki katika juhudi za kuuhifadhi,akisisitiza kuwa kamati itahakikisha mto huo unasafishwa kila mwaka ili kupunguza hatari ya mafuriko.

Mhe. Jackson Kiswagwa (MB), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, akizungumza kando ya Mto Lumemo picha na Kuruthum Mkata
sauti ya Mwenyekiti wa kamati ya Bunge
Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, kwa niaba ya Waziri wa Maji amesema Serikali imepokea na itafanyia kazi ushauri wa kamati hiyo, hususan katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa ili kupunguza hatari ya mafuriko na kuwaondolea wananchi adha inayotokana na mafuriko hayo.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, akizungumza mara baada ya Kukagua Mto Lumemo Ifakara
sauti ya Katibu Mkuu
Kwa upande wake Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Rufiji David Munkyala ametaja kuwa Serikali imetumia shilingi milioni 294 katika maboresho ya Mto Lumemo, huku ipande wa pili wa mto huo ukihitaji zaidi ya shilingi bilioni mbili kuweka tuta ambapo Amesema kazi za maboresho zilizopo katika eneo hilo zinaelekea kukamilika, kwa lengo la kuzuia tatizo la mto kukatika na kupunguza madhara ya mafuriko kwa wananchi wa Ifakara.

Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Rufiji David Munkyala( mwenye Miwani) akitoa uafafanuzi mbele ya kamati ya Bunge picha na Kuruthum Mkata
sauti ya Mkurugenzi wa Bonde
Naye Diwani wa Kata ya Ifakara, Khalfan Mteke, ameiomba Serikali kuhakikisha Mto Lumemo unasafishwa kuanzia mwanzo hadi mwisho ili kuzuia kukatika na kusababisha mafuriko, huku akiishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kuboresha mto huo kwa lengo la kulinda maisha na mali za wananchi.

Diwani wa Kata ya Ifakara, Khalfan Mteke, akielezea changamoto za Mto Lumemo mbele ya kamati ya Kudumu ya Bunge
sauti ya Diwani
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo, akiwemo Amisi Maganga, wameishukuru Serikali kwa hatua za maboresho ya mto huo, huku wakieleza changamoto walizokutana nazo wakati wa mafuriko yaliyosababishwa na kukatika kwa Mto Lumemo.

Mzee Amisi Maganga, Mkazi wa Kata ya Ifakara akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge Picha na Kuruthum Mkata